Home Mchanganyiko NDIKILO ATOA AGIZO KALI KWA KAMPUNI YA ULINZI YA ASLO-PA SECURITY LTD...

NDIKILO ATOA AGIZO KALI KWA KAMPUNI YA ULINZI YA ASLO-PA SECURITY LTD ILIYOPEWA KAZI YA ULINZI NA MKANDARASI KUACHA KAZI HIYO NA IKABIDHIWE KWA SUMA JK

0

***************

NA MWAMVUA MWINYI,KIBAHA
MWENYEKITI wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo ameagiza kampuni ya ulinzi ya Aslo-Pa security service ltd, iliyopewa kazi ya kulinda na mkandarasi katika kiwanda cha Hester Biosciences Africa Ltd, Kibaha,iache kazi hiyo mara moja baada ya kutokea wizi wa nondo tani nne zenye thamani ya milioni kumi.
Aidha ameliagiza jeshi la polisi mkoani humo, lisaidie kuchunguza suala hilo kwani inaonekana kuna ushirikiano wa wizi baina ya baadhi ya walinzi wa kampuni na wengine .
Akitoa maelekezo hayo ,wakati alipokwenda kutembelea kiwanda hicho ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kuweka mawe ya msingi katika viwanda 13, Ndikilo ambae pia ni mkuu wa mkoa wa Pwani ,alielekeza kazi hiyo ya ulinzi ikabidhiwe kwa SumaJkt  .
Ndikilo alitoa rai kwa walinzi na mafundi wanaopewa nafasi ya kulinda na kujenga miradi mikubwa kuwa waaminifu na kuacha udokozi na wizi hali inayosababisha hasara na kuchelewesha kukamilika kwa miradi.
Akizungumzia kiwanda cha Hester alisema kinaenda kuondoa tatizo la ukosefu wa chanjo za mifugo nchini kwani ni kiwanda pekee Tanzania.
“Ni gharama kubwa tunapoteza kuagiza chanjo za wanyama nje ya nchi ,sasa kukamilika kwa kiwanda hiki itaokoa gharama kubwa tunazotumia na wafugaji wa mkoa na Tanzania watanufaika kupatikana kwa madawa haya hapa hapa nchini”alieleza Ndikilo.
Alifafanua ,magonjwa ya wanyama yamekuwa yakirudisha nyuma jitihada za wakulima na wafugaji kwakuwa wamekuwa wakikosa fursa ya soko nje ya nchi kutokana na mifugo kuathirika na magonjwa .
Ndikilo aliutaka uongozi wa kiwanda hicho kujitangaza ,kutangaza uzalishaji wa madawa hayo ya wanyama na chanjo ya magonjwa ya wanyama ili kutambulika.
Awali mratibu wa mradi, Tina Sokoine alisema, ujenzi wa kiwanda utagharimu kiasi cha dollar za kimarekani milioni 18, wanatarajia kuajili wafanyakazi 300 na chanjo itakuwa ikitolewa kwa magonjwa 26 ya wanyama .
Alibainisha, ujenzi umeanza mwaka 2019 na utakamilika Jan 2020 ambapo feb 2020 wanatarajia kuanza kuweka mitambo na kuifanyia majaribio na kutoa elimu kwa wafanyakazi.
Aliomba waongezwe ardhi hekari mbili kwa ajili ya kujenga nyumba za watumishi ili kuepuka wafanyakazi kukaaa nje ya eneo la kazi.
Nae mkuu wa wilaya ya Kibaha ,Assumpter Mshama alisema wana maeneo ya kutosha ,ambapo mji wa Kibaha pia kuna hekari 1,246 eneo la Zegereni.
Assumpter alisema wenye mashamba pori na maeneo yaliyotelekezwa ,taratibu zinafanyika kisheria kuwapokonya na serikali itaangalia shughuli za kufanya ikiwemo za uwekezaji.