Home Mchanganyiko NAIBU WAZIRI MGALU AONGOZA TIMU YA WIZARA NA TAASISI KUWASILISHA TAARIFA KWA...

NAIBU WAZIRI MGALU AONGOZA TIMU YA WIZARA NA TAASISI KUWASILISHA TAARIFA KWA KAMATI YA BUNGE

0

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (kulia), akiongoza kikao cha majumuisho kwa wataalamu kutoka Taasisi zilizo chini yake, mara baada ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dodoma, Agosti 21, 2019. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Haji Janabi.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, akiongoza kikao cha majumuisho kwa wataalamu kutoka Taasisi zilizo chini yake, mara baada ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dodoma, Agosti 21, 2019.

Wataalamu mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake, wakiwa katika kikao cha majumuisho mara baada ya kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dodoma, Agosti 21, 2019.

………………………………

Na Veronica Simba – Dodoma

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, leo Agosti 21, 2019 aliongoza Ujumbe wa wataalamu kutoka wizarani na taasisi zilizo chini yake, kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Taarifa zilizowasilishwa katika kikao hicho ni zinazohusu miradi inayotekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA).

Akiwasilisha taarifa ya shirika lake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt James Mataragio, aliiambia Kamati husika kuwa usambazaji wa gesi asilia majumbani na viwandani umeanza katika maeneo ambayo tayari kuna miundombinu wezeshi. Ametaja maeneo hayo kuwa ni Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam.

“Uunganishwaji wa wateja mbalimbali umefanyika ikiwemo wa viwandani na majumbani ambao wote hutumia gesi kama nishati mbadala,” alieleza.

Dkt. Mataragio, alitaja viwanda ambavyo vimesambaziwa gesi katika mikoa mbalimbali pamoja na vilivyo mbioni kupatiwa huduma hiyo kuwa ni pamoja na Lodhia Steel, kiwanda cha vigae cha Goodwill, Knauf Gypsum, Shreeji Silicates Tanzania Ltd, LN Future Building Material Co. Ltd, Wuzhoe pamoja na Balstian Group of Companies vya Mkuranga mkoani Pwani.

Alisema kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni kiwanda cha Coca Cola, Polypety, Interchick, Chemi & Cortex, ESTIM Construction pamoja na Hoteli zilizopo maeneo ya Mbezi Beach. Aidha, amesema kingine ni kiwanda cha saruji cha Dangote  kilichopo mkoani Mtwara.

Akizungumzia usambazaji wa gesi asilia majumbani, alisema zoezi hilo linaendelea katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara na Lindi na kwamba lengo ni kufikia nyumba za awali 233, Dar es Salaam na 125 Mtwara ifikapo Oktoba mwaka huu.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa PBPA, Erasto Simon, aliieleza Kamati hiyo ya Bunge kuwa matumizi ya gesi ya kupikia kwa hapa nchini yameongezeka kufikia tani 8,000 kwa mwezi kutoka tani 4,000 kwa mwaka mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Alisema serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuboresha biashara na matumizi ya gesi ya kupikia hapa nchini ikiwemo hatua kubwa ya mpango wa kuagiza gesi hiyo kupitia mfumo wa uagizaji kwa pamoja.

“Mfumo huo utasaidia sana katika kupata gharama halisi za uagizaji hivyo kusaidia upangaji wa bei yake nchini, Vilevile, utaongeza ufanisi katika matumizi ya miundombinu ya kupokelea gesi hiyo. Pia, mfumo utasaidia kupungua kwa gharama kutokana na kuagiza kwa pamoja hivyo kupunguza bei yake,” amefafanua.

Kikao hicho ni mfululizo wa vikao vya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini vilivyoanza Agosti 20 na kutarajiwa kukamilika Agosti 24 ambapo Wizara ya Nishati na Taasisi zake zinawasilisha taarifa mbalimbali kuhusu miradi ambayo zinatekeleza.