Home Michezo YANGA INA MATUMAINI YA KUWAONDOA TOWNSHIP ROLLERS JUMAMOSI

YANGA INA MATUMAINI YA KUWAONDOA TOWNSHIP ROLLERS JUMAMOSI

0

Na Mwandishi Wetu, GABORONE
MAKAMU Mwenyekiti wa Yanga SC, Frederick Mwakalebela amesema kwamba wachezaji wana ari kubwa kuelekea mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Township Rollers Jumamosi Uwanja wa Taifa wa Gaborone.
Akizungumza mjini hapa leo, Mwakalebela amesema kwamba kikosi kimefikia katika hoteli ya Crystal Palace mjini hapa kikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Shirikisho la Soka Botswana ambao ni wa nyasi bandia.
“Tunafanya mazoezi kwenye Uwanja wa FA ya huku ambao ni wa nyasi bandia na ni mzuri kabisa na wachezaji wanafirahia. Kwa ujumla wachezaji wana ari kubwa kuelekea mechi hii,”amesema Mwakalebala ambaye pia ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Yanga SC inahitaji ushindi wa ugenini lazima ili kusonga mbele kwenye michuano hiyo, kufuatia kulazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 nyumbani, Jumamosi na Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam. 
Baada ya mchezo wa kwanza mjini Dar es Salaam, Yanga iliweka kambi ya wiki moja mjini Moshi mkoani Kilimanjaro ambako hali yake ya hewa inakaribia kufanana na ya Botswana.
Na ikiwa huko ilicheza mechi mbili za kujipima nguvu, ikifungwa moja 2-0 na wenyeji, Polisi Tanzania Uwanja wa Ushirika mjini Moshi na kushinda moja, 1-0 dhidi ya AFC Leopards ya Kenya Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.