Naibu Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi Dkt. Lewis Ishemoi (aliyesimama) akisisitiza jambo wakati wa kufungua mafunzo ya utozaji kodi katika sekta ya ujenzi kwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo yanafanyika katika Chuo cha Kodi. Waliokaa kutoka kulia:- Mkuu wa Kozi Fupi ITA, Dkt. Amos Ibrahim, Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo cha Kodi Mipango, Fedha na Utawala Emmanuel Masalu, Mwakilishi kutoka JICA Ayako Hatori na Mkufunzi Prof. Ninatubu Lema
Naibu Mkuu wa Chuo cha Kodi (ITA) Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi Dkt. Lewis Ishemoi (waliokaa katikati) katika picha ya pamoja na washiriki na wakufunzi wa mafunzo ya utozaji kodi sekta ya ujenzi mara baada ya kufungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Chuo cha Kodi.
Washiriki wa mafunzo ya utozaji kodi katika sekta ya ujenzi wakifuatilia mada kutoka kwa mkufunzi Prof. Ninatubu Lema
Washiriki wa mafunzo ya utozaji kodi katika sekta ya ujenzi wakifuatilia kwa makini mafunzo ambayo yanafanyika katika Chuo cha Kodi
………………………
Katika jitihada za kuhakikisha kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inakuwa na wataalamu waliobobea katika ukusanyaji wa kodi katika sekta ya ujenzi, Chuo cha Kodi (ITA) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Misaada la Japan (JICA) wameendesha mafunzo ya utozaji kodi katika sekta ya ujenzi kwa watumishi wa TRA.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Chuo cha Kodi, Naibu Mkuu wa Chuo cha Kodi Taaluma Dr. Lewis Ishemoi amesema kwamba mafunzo hayo yataisadia TRA kuongeza makusanyo ya kodi hususan kutoka katika sekta ya ujenzi.
“Mafunzo haya yatawajengea uwezo washiriki ambao ni watumishi wa TRA katika ukusanyaji wa kodi kutoka katika sekta ya ujenzi na kupata uzoefu wa sekta hiyo kutoka kwa wawezeshaji kutoka Japan”, amesema Dr. Ishemoi ambaye ameishukuru serikali ya Japan kupitia shirika lake la kimataifa la Misaada –JICA kwa kufadhili mafunzo hayo pamoja miradi mingine mbalimbali katika kuwajengea uwezo watumishi wa TRA.
Awali akielezea muhtasari wa mafunzo hayo, Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo cha Kodi Mipango, Fedha na Utawala Emmanuel Masalu, amesema kwamba lengo la mafunzo hayo ni kuwasaidia wakufunzi kuuelewa mfumo mzima wa ujenzi pamoja na shughuli muhimu katika sekta hiyo, kufahamu mnyororo wa thamani pamoja na kufahamu wadau wakuu katika shughuli za ujenzi.
“Lengo ni kuielewa vema sekta ya ujenzi ili kutambua vitovu vya kodi katika sekta hiyo kwani ujenzi ni miongoni mwa sekta maalum nchini ambazo zinakua kwa kasi”, amesema Masalu na kuongeza kwamba wakufunzi pia watapata uelewa wa kodi za kimataifa na hivyo kuwa na weledi wa kukusanya kodi za kimataifa kutokana na kuwepo na miradi mingi nchini ambayo inaendeshwa na makampuni ya kimataifa kama vile makampuni ya ujenzi kutoka China na Uturuki.
Pamoja na mafunzo hayo washiriki pia watapata uzoefu wa ukusanyaji kodi katika sekta ya ujenzi kutoka kwa wakufunzi wa Japan nchi ambayo imepiga hatua kubwa katika sekta ya ujenzi.
Mafunzo hayo ya siku tano yanafanyika katika Chuo cha Kodi na kuwashirikisha watumishi wa TRA kutoka katika Mikoa mbalimbali ya kodi. Mafunzo hayo ni muendelezo wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa TRA katika ukusanyaji wa kodi kutoka katika sekta maalum za ujenzi, mawasiliano, madini, mafuta na gesi ambazo zinakua kwa kasi na hivyo kuhitaji wataalamu wa kodi wenye weledi ili kuweza kukusanya kodi stahiki kutoka katika sekta hizo.