Home Uncategorized MAOFISA TARAFA PWANI WAAGIZWA KUDHIBITI KESI ZA MIMBA ZA UTOTONI ZINAZOMALIZWA KIMYA...

MAOFISA TARAFA PWANI WAAGIZWA KUDHIBITI KESI ZA MIMBA ZA UTOTONI ZINAZOMALIZWA KIMYA KIMYA PAMOJA NA KUKAMATA WAPIGA WALE MIMBA-NDIKILO

0

**************

NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
SERIKALI Mkoani Pwani, imewaagiza Maofisa Tarafa mkoani humo, kudhibiti kesi za mimba za utotoni zinazomalizwa kimya kimya pamoja na kusimama kidete kuhakikisha wale wanaohusika kupiga mimba wanafunzi wa kike wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria bila kufanya ajizi.
Aidha amewataka maofisa tarafa hao kutatua na kutafutia ufumbuzi migogoro ya wakulima na wafugaji na ardhi ,kabla wananchi hawajapeleka malalamiko ngazi ya juu .
Akitoa maagizo hayo, wakati akikabidhi pikipiki 28 kwa maofisa tarafa na mkoa, mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo alieleza ofisa Tarafa ni kiongozi muhimu ndani ya serikali lakini cha kushangaza wapo baadhi yao wanashindwa kusimamia na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wanaowapa mimba wanafunzi.
“Tokeni maofisini nendeni mkasimamie majukumu yaliyo kwenye maeneo yenu, kasimamieni tatizo ambalo bado ni kubwa la mimba na utoro mashuleni ,kama haitoshi wapiga mimba ,mnawajua,kamata piga ndani,msiruhusu kesi hizo kuisha kimya kimya”alisisitiza  Ndikilo.
Hata hivyo Ndikilo ,alisema haiwezekani kuhamasisha masuala ya uwekezaji na kuinua sekta ya viwanda wakati migogoro ya ardhi, imesheheni katika maeneo yao.
“Msikae maofisini, katafuteni ufumbuzi wa migogoro ya ardhi shambani, wakulima na wafugaji kakaeni nao pande zote mbili zenye migogoro  ,kamalizeni migogoro ya kijiji kwa kijiji”:File la malalamiko kwa mwezi unakuta migogoro ya ardhi ndio imejaa,sasa maofisa tarafa mpo huko kwanini watu wanafuata suluhu ngazi za juu kabla nyie hamjakaa nao”alisema.
Pia aliwaasa, kufuatilia miradi mikubwa ya maendeleo, kuimarisha ulinzi na usalama na kuhamasisha watu kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Awali akimkaribisha mkuu wa mkoa ,katibu tawala wa mkoa ,Theresia Mbando alisema pikipiki hizo zinakwenda kuleta maendeleo chanya kwakuwa awali kulikuwa na changamoto kwenye baadhi ya maeneo ambapo wengine kutumia pikipiki chakavu za tangu miaka 17 iliyopita.
Nae ofisa tarafa wa Msoga, Mgeni Juma alisema kwa sasa tatizo la usafiri katika majukumu yake ya kikazi linakuwa historia kwani wamepata usafiri wa uhakika.