…………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Patrobass Katambi ametahadharisha kwa baadhi ya watu wanaowarubuni na kuwapatia Mimba watoto wa Shule na kusema kuwa mtu yeyote atakayebainika amempatia Mimba Mtoto wa Kike hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Mhe.Katambi ameyasema hayo jijini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya siku ya vijana Duniani ambayo kwa Tanzania yalianza Agosti 15 na kuhitimishwa Agosti 16 yaliyoenda sambamba na Bonanza la michezo na Matamasha mbalimbali likikutanisha zaidi ya Vijana 500 kutoka Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema mtu akimpatia Mimba mtoto wa shule kuanzia chekechea hadi kidato cha sita atashughulikiwa na kufungwa kwa mujibu wa sheria.
“Kama sheria zilivyo serikali itaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wanaowapatia mimba watoto wa shule,haiwezekani mtoto akose ndoto zake za masomo”amesema Katambi
Aidha ,Katambi amesema kwa upande wa wazazi wanaokubaliana ili wayamalize pindi mtoto wa kike anapopatiwa mimba nao ni wahalifu kama wahalifu wengine na tayari amesema kuna watu wawili wameshafungwa kutokana na kuwapatia mimba watoto wa shule.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya amesema Serikali itaendelea kuheshimu kazi kubwa zinazofanywa na asasi za kimataifa ikiwa ni Pamoja na elimu ya Uzazi ,kuwajali wenye ulemavu,kuwawezesha kiuchumi na kupinga mimba za utotoni.
Mkuu huyo wa Wilaya ameendelea kufafanua kuwa zaidi ya Tsh.Bilioni 2.5 na zaidi katika jiji la Dodoma zimetengwa kwa ajili ya Vijana huku akizungumzia kuanzishwa kwa hospitali tembezi ili kuweza kuwafikia vijana walio wengi na Zaidi ya Tsh.Bilioni 2.9 zimetengwa kwa ajili ya hospitali ya Uhuru.
Pia Mhe.Katambi amesema serikali ipo tayari kuzifutia leseni taasisi ambazo ambazo zimekuwa zikiwezeshwa kwa lengo la kusaidia vijana lakini hazitimizi matakwa hayo.
Meneja Program ya vijana na Maendeleo kutoka UNFPA- Tanzania Dkt.Majaliwa Marwa,amesema UNFPA itaendelea kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na serikali ya Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania ikiwa ni pamoja na kupinga mimba na ndoa za utotoni.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Baraza la vijana Zanzibar Bw.Makoti amesema kuwa serikali zote mbili za Muungano,Bara na visiwani zitaendelea kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali za vijana.
Kilele cha Maadhimisho ya Vijana kimataifa yameenda sambamba na Bonanza na Tamasha la vijana ambao wamejihusisha michezo mbalimbali iliwa ni pamoja na karate,kufukuza kuku,kuvuta kamba,kutembea na ndimu kwa kutumia kijiko mdomoni na uimbaji na kaulimbiu mwaka 2019 ni boresha Elimu.