Home Mchanganyiko MKANDARASI MRADI WA UMEME KINYEREZI 1 EXTENSION ATAKIWA KURUDI ENEO LA KAZI

MKANDARASI MRADI WA UMEME KINYEREZI 1 EXTENSION ATAKIWA KURUDI ENEO LA KAZI

0

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (wa pili kushoto) akikagua mitambo ya umeme ya Kinyerezi jijini Dar es Saalam. Wengine alioambatana nao ni watendaji kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.

Mtaalam kutoka kampuni ya Jacobsen Electric akitoa maelezo kwa Waziri wa Nishati Dkt, Medard Kalemani kuhusu utekelezaji wa mradi wa Kinyerezi 1 Extension.

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani (katikati) akiangalia kazi ya ujenzi wa nguzo za umeme utakaotumika kuendesha Treni za kisasa katika mradi wa SGR.

…………………

Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ametoa agizo kwa Mamlaka zinazosimamia ujenzi wa mradi wa Kinyerezi I Extension (MW 185) kuhakikisha kuwa, mkandarasi wa mradi huo, kampuni ya Jacobsen Electric anarudi katika eneo la kazi na kukamilisha kazi hiyo kwa mujibu wa mkataba.

Dkt Kalemani alitoa kauli hiyo tarehe 13 Agosti, 2019 baada ya kufanya ziara katika eneo la mradi na kuelezwa kuwa wataalam wa kampuni hiyo wameondoka nchini kwa madai kuwa kampuni hiyo imefilisika.

“ Nimefika kukagua kazi hapa na mkandarasi hayupo site, kimsingi wametelekeza mradi, na ni muda sasa kazi za ujenzi haziendelei, hili suala halikubaliki, mimi ninachotaka hapa ni kuona kazi inaendelea na tupate megawati 185 haraka iwezekanavyo.” Alisema Dkt Kalemani.

Aidha, Waziri wa Nishati alihoji kuhusu wasimamizi wa mradi huo kuacha wataalam hao kuondoka nchini bila kuchukua hatua zozote na kuagiza kuwa kazi za ujenzi ziendelee kuanzia leo.

Vilevile, Dkt Kalemani alitoa agizo kuwa, vifaa mbalimbali vya mradi huo vilivyopo bandarini zikiwemo transfoma vitolewe ili kukamilisha mradi huo, na kumuagiza mkandarasi kugharamia kazi hiyo kwani lilikuwa ni jukumu lake kutoka awali.

Dkt. Kalemani pia aliagiza kuwa, mtaalam mmoja wa kampuni hiyo aliyebaki kwenye eneo hilo la kazi, hati  yake ya kusafiria ishikiliwe na Mamlaka zinazohusika mpaka kampuni hiyo itakapomaliza kazi iliyokabidhiwa na Serikali.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati, alikagua kazi ya ujenzi wa nguzo za umeme (kV 220) utakaotumika kuendesha Treni za kisasa katika Reli ya Kisasa ya SGR.

Baada ya ukaguzi wa kazi hiyo inayofanywa na mkandarasi kampuni L& T Construction ya nchini India, aliagiza kuwa kazi hiyo ikamilike kabla ya mwezi Disemba mwaka huu ili mradi huo wa SGR uwe wa mafanikio.

Dkt Kalemani alisema kuwa, jumla ya nguzo za umeme 455 zitajengwa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro hivyo amemtaka mkandarasi kuwa na vibarua wa kutosha na kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha kazi ndani ya wakati.

Mpaka sasa utekelezaji wa mradi wa Kinyerezi I Extension umefikia asilimia 84.

Katika ziara hiyo, Waziri wa Nishati, aliambatana na Kamishna Msaidizi wa Nishati- Maendeleo ya Nishati, Mhandisi Juma Mkobya na watendaji mbalimbali kutoka TANESCO na TRC.