Home Mchanganyiko WANAOKWENDA KINYUME NA BEI ELEKEZI YA SERIKALI WACHUKULIWE HATUA

WANAOKWENDA KINYUME NA BEI ELEKEZI YA SERIKALI WACHUKULIWE HATUA

0

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye akisisitiza jambo wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Dk. Sira Ubwa Mamboya (aliyeketi kulia kwake) alipotembelea makao makuu ya Shirika la Posta Tanzania

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Dk. Sira Ubwa Mamboya (wa pili kushoto) akisikiliza maelezo na kuangalia gari lenye mtambo maalum (halipo pichani) wa kufuatilia matumizi ya masafa kutoka kwa mtaalamu wa TCRA wakati wa ziara yake kwenye taasisi hiyo

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa Dk. Sira Ubwa Mamboya (katikati) akiongea na Bodi na Menejimenti ya Shirika la Posta Tanzania wakati wa ziara yake kwenye taasisi hiyo. Wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye

………………….

Na Prisca Ulomi,Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

Serikali imeielekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuwachukulia hatua wanaokwenda kinyume na bei elekezi ya Serikali na warudishe fedha au kuwapiga faini. 

Maelekezo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa ziara ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mheshimiwa Dk. Sira Ubwa Mamboya alipotembelea TCRA ikiwa ni moja ya taasisi ya mawasiliano alizotembelea Tanzania Bara ili kujifunza utendaji kazi wake kwa kuwa mawasiliano ni suala la Muungano ambapo Nditiye ni mwenyeji wa ugeni huo

Nditiye amesema kuwa mwishoni mwa mwaka jana, Serikali ilitoa bei elekezi kwa kampuni za simu za mkononi wakati wa uzinduzi wa Mwongozo wa Watumiaji wa Huduma na Bidhaa za Mawasiliano kuwa ifikapo Januari mosi mwaka huu 2019, gharama ya kupiga simu kutoka mtandao mmoja kwenda mtandao mwingine itakuwa ni shilingi 10.40 kwa dakika moja na sio kwa sekunde kwa kuwa tulikuwa tumetoka shilingi 15.60 kwa dakika moja.

Ameongeza kuwa lakini mpaka sasa hivi huwa nasikia matangazo kutoka kampuni za mawasiliano za simu wanajinadi kuwa kupiga simu mtandao wowote ni shilingi moja kwa sekunde ina maana ukipiga sekunde sitini ni shilingi sitini na inakuwa imezidi mara tano ya gharama ambayo ni mwongozo wa Serikali kwa makampuni ya simu

“Nawataka TCRA sasa waanze kufuatilia makampuni yote ambayo yamekwenda kinyume na bei elekezi ya Serikali, kwanza, wachukue hatua za kinidhamu na wawapige faini lakini wahakikishe hela yetu ambayo hayo makampuni wamekuwa wakichukua isivyo halali inarudi kwa sababu mpango wa Serikali ni kwamba inapofika mwaka 2022 iwe shilingi mbili kwa dakika kupiga mtandao wowote wa simu,” amesisitiza Nditiye.

Nditiye ameipongeza TCRA kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha kuwa Sekta ya Mawasiliano inakuwa juu sana nchini kwetu na tukumbuke kuwa Sekta ya Mawasiliano kupitia wadau kama TCRA tumeweza kwa miaka mitatu mfululizo kuchukua nafasi tatu za mwanzo kuchangia pato kwenye Serikali yetu na tunachangia pato kubwa sana lakini nikawambusha TCRA kuwa bado kuna maeneo ambayo wakiyafanyia kazi vizuri ya kiudhibiti tunaweza tukawa wa kwanza tena bila mashaka yeyote.

Pia, ametoa msisitizo kwa watanzania wajisajii kwa alama za vidole kwa kuwa lengo la Serikali ni zuri na tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuongeza muda hadi mwisho wa mwaka huu watanzania wawe wamejisajili kwa alama za vidole ili kwanza tuwalinde na waweze kufanya miamala mbali mbali wakiwa na uhakika na hatutaki wala hatupendi tuone mtu mmoja ana miliki laini 160 na zaidi za nini

“Ila tunategemea angalau mtanzania amiliki laini chache alizozisajili kwa kila mtandao atakaopenda ili tumjue ni yeye na itakapofika mwisho wa muda ambao umepangwa tutazima laini zote ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole nia ni kwamba anayepigiwa au anayepiga tumtambue,”amesisitiza Nditiye. 

Pia, ameyataka makampuni ya simu yazingatie na kutoa matangazo ya kitaifa ya kimkakati kama vile homa ya ini na ugonjwa wa UKIMWI kwa kuwa bado upo

Nditiye amesema kuwa Sekta ya Mawasiliano ni ya Muungano hivyo amemshukuru Dkt. Mamboya kwa kuja na amejifunza mambo mengi ikiwemo ukuaji, uendeshaji na udhibiti wa Sekta ya Mawasiliano nchini na amemkaribisha Dkt. Mamboya kuja Tanzania Bara popote pale na akijisikia kwenda kukagua mawasiliano aende iwe Mtwara, Bukoba, Katavi na awe huru kama ambavyo huwa naenda Unguja na Pemba kushughulikia  masuala ya mawasiliano 

Katika hatua nyingine, ugeni huo ulitembelea Shirika la Posta Tanzania (TPC) ambapo Dkt. Mamboya ameipongeza TPC kwa kutoa gawio na kwa ujasiri na utayari wa kuendelea kutoa huduma kwa wananchi. Pia, ameipongeza Bodi ya TPC kwa kuwa imara kwa kuwa ukiwa na Bodi legelege hakuna mafanikio ya taasisi na hamuwezi kutoa gawio. Nditiye kwa upande wake ameitaka TPC kutangaza huduma zake mara kwa mara na kuchamkia fursa zilizopo kwa kuhudumia wananchi kwa kuwasogezea huduma na bidhaa karibu nao