Home Mchanganyiko Mloganzila Kufungua Benki za Maziwa ya Mama kwa Ajili ya Watoto Wachanga

Mloganzila Kufungua Benki za Maziwa ya Mama kwa Ajili ya Watoto Wachanga

0
Mtaalam wa lishe katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Bi. Theresia Thomas akiwafundisha wazazi umuhimu wa unyonyeshaji na uandaaji wa chakula cha watoto kuanzia miezi sita mpaka miaka miwili katika maadhimisho ya siku ya unyonyeshaji duniani ambayo huadhimishwa tarehe 1 hadi 7 Agosti, kila mwaka.
Mtaalam wa lishe Bi. Prisca Emmanuel (kulia) akimpima hali ya lishe mtoto Brightness Temba, aliyembeba mtoto ni Bw. Emily Temba.
 Mtaalam wa lishe Bi. Arafa Mkumbo akimpima uzito na urefu mtoto Aria Madari ili kujua hali yake ya lishe ikiwa ni maadhimisho ya siku ya unyonyeshaji duniani ambapo Hospitali ya Mloganzila imetoa bure huduma ya upimaji wa hali ya lishe kwa watoto chini ya miaka mitano, ushauri wa lishe, miongozo ya uandaaji wa chakula cha watoto pamoja na elimu ya umuhimu wa unyonyeshaji kwa watu wote.
 Baadhi ya wazazi ambao wamejitokeza leo kwa ajili ya kupata huduma ya upimaji wa hali ya lishe kwa watoto chini ya miaka mitano, ushauri wa lishe, miongozo ya uandaaji wa chakula cha watoto pamoja na elimu ya umuhimu wa unyonyeshaji.
………………………..
Hospitali ya Taifa Muhimbili – Mloganzila inatarajia kufungua benki za maziwa ya mama kwa lengo la kusisitiza umuhimu wa kuwapatia watoto wachanga maziwa ya mama ambayo ni chakula bora na salama.
Hivyo kina mama watakojifungua katika Hospitali ya Muhimbili watahimizwa kutoa maziwa yao ambayo yatatunzwa na kutumiwa na watoto wachanga wote waliozaliwa kwa wakati huo wakiwemo watoto ambao mama zao wamefariki au mama hatoi maziwa.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru wakati akizungumzia kuhusu maadhimisho ya siku ya unyonyeshaji duniani ambapo Hospitali ya Mloganzila imetoa bure huduma ya upimaji wa hali ya lishe kwa watoto chini ya miaka mitano, ushauri wa lishe, miongozo ya uandaaji wa chakula cha watoto pamoja na elimu ya umuhimu wa unyonyeshaji kwa watu wote.
Amesema nia ya serikali ni kwamba zitakapofunguliwa benki za maziwa Muhimbili baadaye huduma hiyo itaenea nchi nzima ambapo hospitali mbambali nazo zitatakiwa zifungue benki hizo kwa ajili ya kuwapatia maziwa ya mama watoto wachanga waliopo hospitalini.
“Tunaamini katika hili pia mama aliyeko nyumbani endapo anashughuli zake anaweza kutoa maziwa yake akayaweka muda ukifika wa kunyonyesha mtoto atanyonyeshwa na yule aliyepo huku mama akiendelea na shughuli nyingine” amesema Prof. Museru.
Baadhi ya faida za unyonyeshaji ni, maziwa ya mama yana maji na virutubisho vyote muhimu hivyo husaidia mtoto kukua vizuri mwili na akili, huimarisha kinga ya mwili wa mtoto na kumkinga dhidi ya magonjwa pia maziwa ya mama ni safi, salama na yana joo linalofaa.
Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji yalianza mwaka 1992 mpaka sasa takribani nchi 120 ni wafuasi wa siku hii duniani ambapo, huadhimishwa kwa lengo la kuhamasisha, kulinda na kuwezesha unyonyeshaji wa watoto ndani ya saa moja anapozaliwa mpaka miaka miwili ili kufanya ukuaji bora na wenye tija.