Home Mchanganyiko DC NJOMBE AMALIZA MGOGORO WA ARDHI KIJIJI CHA KILENZI

DC NJOMBE AMALIZA MGOGORO WA ARDHI KIJIJI CHA KILENZI

0
NJOMBE.

Mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri amemaliza mgogoro wa ardhi katika kijiji cha Kilenzi tarafa ya Igominyi katika halmashauri ya mji wa Njombe uliyodumu kwa zaidi ya miaka 3 baada ya wanakijiji watatu kuvamia eneo la machungio kwa shughuli binafsi kikiwemo kilimo na ufugaji.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara mara baada ya kuketi na upade wa watuhumiwa akiwemo Beno Mdetele ,Ibrahim Mdetele na Onoratus Mdetele pamoja na upande wa serikali ya kijiji mkuu huyo wa wilaya amesema baada ya kupokea malalamiko miezi kadhaa alilazimika kutuma kikosi cha wataalamu kwenda kupima eneo lililovamiwa na kubaini kuwa eneo lenye ukubwa wa ekari 26 lilitolewa kimakosa kwa watu hao na vizazi vilivyotangulia pamoja na serikali ya kijiji hicho kabla hakija gawanyika.

Kutokana na hali hiyo serikali imekuja na agizo la kuwataka wavamizi wote kulirudisha eneo hilo katika serikali ya kijiji ili liweze kutumika kama watangulizi walivyokusudia huku pia akitoa agizo kwa serikali ya kijiji kupanda miti rafiki katika eneo oevu linalopitiwa na mkondo wa maji katika eneo hilo na kuondoa miti ya mbao iliyopandwa na wavamizi.

Baada ya ukweli kujulikana juu ya mmiliki halali wa eneo hilo la machungio ambalo lilivamiwa na watu watatu mkuu wa wilaya anawataka wavamizi hao kutoka mbele ya mkutano na kujieleza iwapo wameridhia kuachia ardhi waliyovamia kwa madai ya kwamba walipewa na wazazi wao na mengine kupatiwa na serikali ya kijiji ambapo wanasema wamekubali kurejesha kijijini ardhi hiyo ili kurejesha amani.

Kwa upande wao wakazi wa kijiji cha kilenzi ambao wanasema walikosa kabisa eneo la kuchunga na kulisha mifugo yao kipindi eneo hilo lilipokuwa chini ya wavamizi hao na kwamba maridhiano yaliofanyika yamenusuru mifugo yao.