Home Mchanganyiko WAFANYABIASHARA WEKEZENI KWENYE VIWANDA VYA MAFUTA YA KULA NA SUKARI-MHE HASUNGA

WAFANYABIASHARA WEKEZENI KWENYE VIWANDA VYA MAFUTA YA KULA NA SUKARI-MHE HASUNGA

0

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Kushoto) akiwa na Waziri Mkuu mstaafu wa awamu ya nne Mhe Mizengo Pinda (Katikati) wakati wa ukaguzi wa mabanda ya maonesho ya wakulima (Nanenane) kwenye hafla ya ufunguzi wa kongamano la fursa za Kilimo biashara katika viwanja vya Nyakabindi katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu. Mwingine pichani ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu Ndg Jumanne Sagini. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa kongamano la fursa za Kilimo biashara kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi ambaye ni Waziri Mkuu mstaafu wa serikali ya awamu ya nne Mhe Mizengo Pinda katika viwanja vya Nyakabindi Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwenye maonesho ya wakulima (Nanenane) yanayofanyika kitaifa mkoani Simiyu. 
Sehemu ya wananchi waliojitokeza kwenye hafla ya ufunguzi wa kongamano la fursa za Kilimo biashara wakifatilia kwa makini kongamano hilo kwa makini katika viwanja vya Nyakabindi Halmashauri ya Mji wa Bariadi kwenye maonesho ya wakulima (Nanenane) yanayofanyika kitaifa mkoani Simiyu. 
Na Mathias Canal, Wizara ya
Kilimo-Simiyu
Wafanyabiashara nchini
Tanzania na nje ya nchi wametakiwa kuwekeza katika viwanda vya uchakataji wa
mazao mbalimbali yakiwemo miwa na alizeti.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet
Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo Tarehe 6 Agosti 2019 wakati akizungumza kwenye
hafla ya ufunguzi wa kongamano la fursa za Kilimo biashara katika viwanja vya
Nyakabindi kwenye maonesho ya Sikukuu ya wakulima (Nanenane) katika Halmashauri
ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu.
Mhe Hasunga amesema kuwa
endapo wakulima watawekeza katika Kilimo cha alizeti ni wazi kuwa wataimarisha
upatikanaji wa mafuta ya kula yanayotokana na zao hilo hivyo kuondokana na
dhana ya uagizaji wa mafuta kutoka nje ya nchi.
Alisema kuwa Tanzania
inauhitaji wa mafuta ya kula kiasi cha Tani 570,000 lakini pamoja na kuwa na
ardhi nzuri na yenye rutuba lakini juhudi za uzalishaji bado ni ndogo kwani
kama nchi inazalisha Tani 250,000 pekee.
Alisema kuwa kiasi cha
Bilioni 678 zilitumika mwaka 2018 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi
ilihali kuna uwezo wa kuzalisha kwa wingi zao hilo na fedha ambazo zinatumika
kuagiza  zingeweza kutumika katika kutekeleza miradi mingine.
Kuhusu Sukari, Waziri huyo
wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga amesema kuwa Tanzania ina uhitaji wa sukari kiasi
cha Tani 675,000 ambapo Tani 175,000 kati ya hizo ni sukari za viwandani
ilihali kiasi kilichosalia ni sukari ya kawaida, lakini uwezo wa nchi ni
kuzalisha Tani 359,000 pekee.
Alisema kuwa ni jambo la
ajabu kuagiza sukari nje ya nchi  kwa kutumia gharama kubwa ilihali kuna
maeneo mazuri kwa ajili ya kilimo na kuzalisha miwa.
Aidha, amewasihi wakulima
kuzalisha miwa kwa wingi kwani ni miongoni mwa mazao yanayohitajika zaidi
katika biashara sambamba na kufanya mabadiliko katika sekta ya Kilimo kupitia
mkazo wa Programu ya kuendeleza sekta ya Kilimo awamu ya pili (ASDP II).
Kongamano hilo la fursa za
Kilimo biashara katika viwanja vya Nyakabindi kwenye maonesho ya Sikukuu ya
wakulima (Nanenane) katika Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu
limefunguliwa na Waziri Mkuu mstaafu wa serikali ya awamu ya nne ambaye ni
mjumbe wa kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa Mhe Mizengo Peter Pinda.
MWISHO