Home Mchanganyiko DKT. MWANJELWA ATEMBELEA MKOA WA KAGERA KUKAGUA MIRADI YA TASAF

DKT. MWANJELWA ATEMBELEA MKOA WA KAGERA KUKAGUA MIRADI YA TASAF

0

 Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) akizungumza na Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini
(hawapo pichani) katika Manispaa ya Bukoba wakati wa ziara ya kikazi yenye kwa
lengo la kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF na kukutana na Watumishi wa
Umma kuhimiza uwajibikaji.

 Baadhi ya Wanufaika
wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera
wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) (hayupo pichani) alipowatembelea
kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF. 

 Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) akikaribishwa na mmoja wa Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya
Maskini, Manispaa ya Bukoba, Bibi Irene Mgongo katika nyumba aliyoijenga baada
ya kupata ruzuku ya TASAF.

Naibu Waziri, Ofisi
ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary
Mwanjelwa (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na moja ya kaya za Wanufaika wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, Manispaa ya Bukoba.

 

 Mmoja wa Wanufaika wa
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, Manispaa ya Bukoba, Bibi Irene Mgongo
akimuonyesha Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) shamba analolima kwa kutumia ruzuku
ya TASAF ili kujiongezea kipato.

 

 

DKT. MWANJELWA AWAFUNDA WALENGWA WA TASAF MKOANI KAGERA.

 

Na Estom Sanga- Kagera. 

 

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mhe. Dokta Mary Mwanjelwa amewahimiza Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF kuthamini mchango huo wa serikali kwa kufanya kazi kwa bidii ili waweze kunufaika zaidi na kuboresha maisha yao. 

 

Akizungumza kwa nyakati tofauti mwanzoni mwa ziara yake ya mkoani Kagera ambako amekutana na Walengwa wa TASAF na Watumishi wa Umma ,Dr. Mwanjelwa amesema Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wanapaswa kutumia vizuri fursa hiyo adhimu waliyoipata ili waweze kuendelea kunufaika nayo kwa ukamilifu. 

 

Naibu Waziri huyo wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, amesema utekelezaji wa Mpango huo ni miongoni mwa Mikakati ya Serikali ya kukabiliana na kero ya umaskini kwa Wananchi na hivyo akawahimiza kuitumia fursa hiyo kwa kuanzisha miradi ya kujiongezea kipato na kukuza uchumi wao na taifa kwa jumla. 

 

Aidha Dr. Mwanjelwa amepongeza mafanikio yaliyoanza kuonekana kwa Walengwa wa TASAF kuanza kuboresha maisha yao kwa kujenga nyumba,kuanzisha miradi ya kilimo, ufugaji na kukuza sekta ya elimu na afya ambayo amesema kwa kiwango kikubwa zimesaidia kukuza uwezo wa kuendesha maisha yao. 

 

Akizungumzia suala la baadhi ya vijiji kutojumuishwa kwenye Mpango, Dr, Mwanjelwa amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dr. John Magufuli ameagiza vijiji vyote vyenye Wananchi wanaostahili kujumuishwa kwenye Mpango huo vipewe fursa hi katika sehemu ya pili ya Mpango wa kunusuru Kaya Maskini inayotarajiwa kuanza hivi karibuni. 

 

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwanjelwa ameonyesha kuridhishwa kwake na mafanikio waliyoanza kupata Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Manispaa ya Bukoba tangu kuanza kutekelezwa kwa Mpango huo hususani katika nyanja za elimu, afya, uzalishaji mali na uboreshaji wa makazi yaa. 

 

“Nimejionea namna walengwa wa TASAF mnavyotumia rukuzu mnayopata kuboresha maisha yenu hilo ni jambo zuri kwani mnaunga mkono nia njema ya serikali ya Awamu ya Tano kwa vitendo,” Amesisitiza Dkt. Mwanjelwa. 

 

Amesema, kwa kutambua mchango wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika maendeleo ya wananchi, Serikali imeamua kuendelea kuutekeleza Mpango huo katika sehemu ya pili ambapo mkazo utawekwa zaidi katika miradi itakayowawezesha Walengwa kufanya kazi katika miradi watakayoibua kwenye maeneo yao na kupata ujira kama njia mojawapo ya kuwaongezea kipato. 

 

Akizungumzia suala la baadhi ya maeneo kutonufaika na huduma za Mpango huo , Naibu Waziri huyo amesema, Serikali imeamua kuwa katika sehemu ya pili ya Mpango huo inayotarajiwa kuanza hivi karibuni maeneo yote nchini ambako wananchi watakidhi vigezo wajumuishwe kwenye huduma za Mpango huo. 

 

“ Serikali hii haibagui wananchi wake, hivyo wale wote ambao watakidhi vigezo vya kuweko kwenye Mpango watapata fursa hiyo ili waweze kuitumia katika kuboresha maisha yao” Amefafanua Dkt Mwanjelwa. 

 

Dkt. Mwanjelwa yuko mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi kujionea utekelezaji wa shughuli za TASAF na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma katika Halmashauri zote za mkoa huo. 

 

Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF- inatekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambapo takribani Kaya za Walengwa zipatazo Milioni MOJA na LAKI MOJA zimenufaika na huduma za Mpango huo katika sehemu yake ya Kwanza iliyoanza kutekelezwa mwaka 2012 kote Tanzania Bara,Unguja na Pemba.