Home Biashara NMB yauza Hati Fungani za Bil.83.3/-

NMB yauza Hati Fungani za Bil.83.3/-

0

Afisa Mkuu wa Wateja Wadogo na wa Kati Benki ya NMB – Filbert Mponzi akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa kutangaza matokeo ya hati fungani ya Benki hiyo katika ofisi za NMB jana jijini Dar es Salaam. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa NMB – Ruth Zaipuna.

Afisa Mkuu wa Fedha, Ruth Zaipuna akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa kutangaza matokeo ya hati fungani ya Benki hiyo katika ofisi za NMB jana jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Ofisa Mkuu wateja wadogo na wakati (Chief Retail Banking), Filbert Mponzi na Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko ya Fedha (Head, Global Markets Treasury department), Gladness Deogratius.

***********

NA MWANDISHI WETU

BENKI ya NMB, imetangaza matokeo ya mauzo ya toleo la tatu la
programu ya hati fungani ya benki hiyo, ambako imekusanya Sh. Bilioni
83.3 sawa na asilimia 333 ya mauzo yaliyotarajiwa awali ya Sh. Bilioni 25.
Mauzo ya toleo la tatu la hati fungani ya NMB yalifunguliwa Juni 10 na
kufungwa Julai 8, mwaka huu, ambako kipindi hicho cha miezi miwili,
kilikuja baada ya Mamlaka ya Masoko na Mitaji na Dhamana (CMSA),
kutoa idhini ya mauzo hayo.

Akizungumza katika hafla ya kutangaza matokeo hayo, iliyofanyika jijini
Dar es Salaam jana, Afisa Mkuu wa Fedha , Ruth Zaipuna, alisema wao
kama benki wanajivunia kiwango hicho cha mauzo, kinachothibitisha
imani ya wananchi na jamii kwa benki yake.

Zaipuna alibainisha kuwa, tayari NMB imeyapokea na kuyakubali maombi
yote na kwamba waombaji wote wa manunuzi ya hati fungani
wametaarifiwa na kwamba leo Agosti 2, wanaorodhesha hati fungani
zote, kabla ya wanunuzi kukabidhiwa vyeti mwezi mmoja ujao.

Alifafanua ya kwamba, mauzo hayo ya kiwango cha juu kuliko
walivyotarajia, yanaiongezea benki nguvu ya kiuchumi katika kufanikisha
utoaji wa mikopo kwa wateja wao na kwamba mchakato mzima
umeshirikisha zaidi ya matawi 200 kote nchini.

“NMB inatoa shukrani za dhati kwa taasisi zote zilizofanikisha uuzwaji wa
toleo la tatu la hati fungani ya NMB, ikiwemo CMSA, Soko la Hisa la Dar es
Salaam (DSE), Mshauri Kiongozi wa NMB, Stanbic Bank Tanzania Ltd na
Dalali Mfadhili wa NMB, Orbit Securities Company Ltd,” alisema Zaipuna.

Hati fungani ni aina ya uwekezaji, ambao unamuwezesha mteja kuwekeza
pesa katika taasisi (hasa shirika la kibiashara au Serikali), kwa kuikopesha
fedha kwa muda maalum na kwa riba isiyobadilika. Riba ya hati fungani
za NMB kwa mwaka ni asilimia 10.

Mteja anaponunua Hati Fungani ya NMB, anakuwa ameikopesha benki
fedha zake, ambako NMB inaahidi kurejesha fedha zake (msingi) katika kipindi maalum cha ukomavu. Kuanzia muda uliowekeza hadi muda wa
ukomavu ambao unakuwa miaka mitatu.