Home Mchanganyiko SERIKALI YANUNUA MAGARI 12 YA HUDUMA YA DHARURA NA UOKOZI

SERIKALI YANUNUA MAGARI 12 YA HUDUMA YA DHARURA NA UOKOZI

0

Mkuu wa kitengo cha afya uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwl.Julius Nyerere George Ndaki akimuonesha ufanyaji kazi wa mashine za kupima joto(thermo scanner) Naibu Waziri Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile wakati alipotembelea eneo la wasafiri wanaoenda nje ya nchi zilizofungwa kwenye uwanja mpya wa ndege terminal three.

Naibu Waziri Dkt.Faustine Ndugulile akionesha kadi za homa ya manjano”Yelow Fever” ambazo zinatolewa na wizara ambapo wizara imefunga kifaa maalum cha kubaini kadi feki ambazo wasafiri huzinunua bila kuchanjwa chanjo hiyo.

Dkt.Ndugulile akioneshwa utofauti wa kadi halisi na kadi feki za homa ya manjano.Dkt.Ndugulile amewasihi wananchi wanaotarajia kusafiri nje ya nchi kuacha kununua kadi feki bali kuhakikisha wanapata chanjo hiyo kwenye vituo rasmi vilivyoelekezwa na wizara ya Afya.

Naibu Waziri akikagua vifaa vingine vilivyofungwa terminal three kwa ajili ya kubaini wahisiwa wa Ebola.

Katika kuelekea Mkutano wa Kimataifa wa SADC wizara ya afya imejipanga kukabiliana na dharura kwa wageni watakaoshiriki mkutano huo.Pichani.Dkt.Ndugulile akikagua magari ya wagonjwa wa dharura yaliyopo ofisi za Toyota.

Naibu Waziri akikagua moja ya chumba cha dharura kilichoandaliwa kwenye hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya washiriki wa mkutano wa SADC.

Mkuu wa Kitengo cha Dharura Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt.Juma Mfinanga (kulia)akimueleza jambo Naibu Waziri wakati alipotembelea kujionea hali ya utayari ya kuwahudumia washiriki wa mkutano wa SADC ambao watapata dharura na hivyo kupatiwa huduma za afya kwenye hospitali hiyo.

************

NA.Catherine Sungura,WAMJW-DSM

Serikali kupitia Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imenunua magari kumi na mbili kwa ajili ya huduma za dharura nchini.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa wizara hiyo Dkt.Faustine Ndugulile wakati alipofanya ukaguzi kwenye ofisi za Toyota jijini hapa.

Dkt.Ndugulile amesema magari hayo yameletwa muda muafa ikiwa zimesalia siku chache kuanza mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo magari hayo pamoja na mabasi mawili ya uokozi yatatumika kutoa huduma za kiafya kwenye mkutano huo na baada ya hapo yatagaiwa kwenye maeneo yaliyoanishwa kwa uokoaji wa majeruhi wa ajali.

“Magari na Mabasi hayo yatatumika kwenye mkutano wa SADC na baadae yatasambazwa katika vituo vya dharura nje ya hospitali ambapo yatatumika kusafirishia majeruhi pindi ajali inapokuwa imetoka.

“Tutayatumia katika mkutano wa SADC, pamoja na ambulance hizo 12 kuna mabasi makubwa mawili ambayo yana huduma zote za msingi ndani ambapo watu wapatao 20 wanaweza kubebwa na kupatiwa msaada wa ajali,” alisema.

Alisema serikali imejipanga pia katika njia ya anga kwa kutumia ndege pindi mtu anapohitaji huduma ya dharura kupelekwa haraka katika eneo jingine hususani hospitali ya Taifa Muhimbili.

“Ni utaratibu ambao Serikali inauweka kuhakikisha waathirika wa ajali wanapata huduma za dharura na ajali, mapema iwezekano na tunasema ndani ya masaa yaliyowekwa ya kuwahudumia majeruhi,” alisema Dkt.Ndugulile

Naibu Waziri huyo alisema wameagiza magari ya zimamoto na uokozi kwamba si tu liwe na uwezo wa kuzima moto bali linakuwa na vifaa vya kisasa, kwa mfano ikiwa gari limepata ajali, milango inashindwa kufunguka, iweze kukatwa ili kuokoa majeruhi, iwezekane.

“Haya ni maendeleo makubwa kwa Serikali katika kuhakikisha majeruhi wanapata huduma za dharura za awali mapema inavyowezekana, kwani wengi hufariki dunia kwa sababu hukosa zile huduma za awali za dharura katika lile li-saa limoja la kwanza,” alisema.

Dk. Ndugulile aliongeza “Inawezekana anavuja damu, anashindwa kupumua vizuri, tuna imani magari, mabasi na mafunzo tuliyowapa wataalamu huduma hizi zitaimarika.

“Natoa rai kwa wananchi, kwani nao wamekuwa wakichangia madhara kwa majeruhi, wanawamalizia wale majeruhi, wakiamini wanawasaidia kuokoa maisha.

“Wahakikishe tu wanamtoa majeruhi na kumuweka pahala pengine mbali na tukio la ajali, kama gari litaweza kulipuka moto ule usimfikie, tunapowabeba ‘mzobe mzobe’ tunawasababishia madhara zaidi.

“Muhimu tuhakikishe huduma za msingi zinapatikana pale pale, kikubwa ni kuhakikisha yule Mgonjwa anapumua, havuji Damu kwa wingi na njia yake ya Hewa IPO salama.

“Jambo la msingi si kumkimbiza majeruhi hospitalini kwanza bali ‘kum-stablize’ pale pale eneo la tukio, kama mfupa umevunjika afunge vizuri usining’ingine, abebwe vizuri kama mshipa wa shingo umevunjika usimalizike, kwani wengi kutokana na ule ubebaji huishia kupooza mwili na hata kufa,” alisema.

Sambamba na hilo, mapema asubuhi, Dk. Ndugulile alifanya ziara kwenye kitengo cha afya ndani ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA- terminal III), kujionea hali ya utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Ebola.