MWENGE wa uhuru ,umekataa kuzindua mradi wa maji Bokomnemela,Kibaha Vijijini,mkoani Pwani baada ya kubaini taratibu za ujenzi kukiukwa katika zege la juu lililotengewa kiasi cha sh.milioni 1.5.#
Aidha kamanda wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), wilayani Kibaha Vijijini amepewa wiki mbili kuufuatilia na kuchunguza kwa kina juu ya mapungufu yaliyoyabainika kisha baada ya uchunguzi taarifa zipelekwe Makao Makuu ya TAKUKURU na afikishiwe taarifa.
Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi wa mradi huo,kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa 2019 ,Mzee Mkongea Ali alisema ,pia mfuniko upo taabani,hali mbaya kiusalama na ngazi za ndani ndani nazo ni tatizo .
“Tumefanya ukaguzi, tumebaini mfuniko haupo kiusalama,akitokea mtu asiyependa maendeleo anaweza kuweka vitu vibaya,tunaomba jitihada za makusudi zichukuliwe ili kurekebisha mapungufu hayo”
“Fedha ya zege la juu imetengwa milioni 1.5 na katika taarifa inaonyesha imelipwa yote,vipimo vipo vitatu kwanini hiki kimoja kisifanyike ,kipimo cha zege la juu hakuna ,kutokana na hili mwenge wa uhuru hauwezi kuzindua mradi huu'”alisisitiza Mkongea.
Mkongea alieleza kuwa, huwa wakipitia miradi ,wanaomba taarifa na kujiridhisha kwakuwa fedha zinazotumika kwenye miradi ni za serikali na kodi za wananchi hivyo inapaswa zisimamiwe vizuri.
“Tunamshukuru Rais dkt .John Magufuli kwa kazi anayoifanya ,”:Kwenye miradi ya maji sisi sote mashahidi tunajionea miradi ya milioni 400,kuna mradi wa jiji la Arusha,mradi wa miji ,Chalinze,Same,Mwanga na Korogwe”alisema Mkongea.
Aliwataka wananchi waendelee kutumia maji kupitia mradi huo kwakuwa vipimo vinaonyesha ni safi na salama.
Kwa upande wake, mhandisi wa maji Kibaha injinia Rebman Ganshonga alifafanua mradi huo unagharama ya sh.milioni 459.458.0 ambao uliibuliwa ili kuhudumia vijiji vitatu ikiwemo Mkarambati,Mnemela Kibaoni na Bokomnemela na watu 6,000.
Ganshonga alibainisha,DAWASA imefanya maboresho makubwa kwenye chanzo cha maji cha Ruvu ambayo yamewezesha kuongezeka kwa msukumo wa maji kutoka 1.5 bar hadi kufikia 3.5 bar hivyo kufanya maji kuwa na uwezo wa kufikia maeneo yote yenye vituo vya kuchotea maji bila kupitia tanki la kuhifadhia maji.
Awali akipokea mwenge wa uhuru ukitokea Bagamoyo,mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama alisema, miradi iliyotembelewa ni Tisa yenye thamani ya sh.bilioni 4.121.