Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua darasa wakati alipotembelea Shule ya Sekondari ya Liuguru wilayani Ruangwa Julai 29, 2019. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Andrew Chezue. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye Shule ya Sekondari ya Liuguru wilayani Ruangwa kukagua majengo ya Shule hiyo na kuzungumza na wananchi, Julai 29, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Liuguru wilayani Ruangwa, Julai 29, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitembelea jengo la wazazi wakati alipokagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa, Julai 29, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Ruangwa kwenye eneo la Nachingwea , Julai 29, 2019. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Andrew Chezue, wakati alipowasili kwenye eneo la Nachingwea kukagua ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Ruangwa, Julai 29, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
****************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa na ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo.
Waziri Mkuu ambaye ni mbunge wa jimbo la Ruangwa na yuko jimboni kwake kwa mapumziko mafupi, alikagua ujenzi huo jana jioni (Jumatatu, Julai 29, 2019). Jengo hilo linalojengwa na SUMA JKT, linahitaji sh. bilioni 3.77 hadi kukamilika kwake.
Akiwa kwenye eneo la ofisi hizo, Waziri Mkuu alielezwa kwamba Halmashauri hiyo imepokea shilingi milioni 500 kutoka Serikali Kuu kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mpya ya Halmashauri hiyo.
Ujenzi wa ofisi hiyo ambayo ikikamilika itakuwa na ghorofa moja, ulianza Juni mosi, 2019 na unatarajiwa kukamilika Julai, mwakani. Jengo litakuwa na ofisi 33 za chini, ofisi 26 za ghorofa ya kwanza na kumbi mbili za mikutano.
Kazi ambazo zimeshafanyika hadi sasa ni usafishaji wa eneo kwa ajili ya ujenzi; upimaji wa sampuli ya udongo (Geotech Survey); uingizaji wa maji eneo la ujenzi; uchimbaji wa kisima kikubwa cha kuhifadhia maji na uvutaji wa umeme eneo la ujenzi.
Kazi zinazoendelea kwa sasa ni ufyatuaji wa tofali ambapo hadi sasa jumla ya matofali 10,000 yamekwishafyatuliwa ambayo ni sawa na asilimia 50 ya mahitaji ya matofali yote. Pia ukusanyaji wa vifaa vya ujenzi eneo la ujenzi unaendelea.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu jana alikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo na kukiri kwamba ameridhishwa na kazi iliyokwishafanyika hadi sasa.
Akiwa hospitalini hapo, Waziri Mkuu alielezwa na Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt. Mahela Njile kwamba hadi kukamilika kwake, hospitali hiyo itakuwa na majengo 22 yanayokisiwa kugharimu jumla ya sh. bilioni 7.5 kulingana na maksio ya OR-TAMISEMI.
Dkt. Njile alisema katika awamu ya kwanza Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 na kuelekeza yajengwe majengo saba ya kipaumbele ambayo ni jengo la uzazi, la wagonjwa wa nje (OPD), maabara, la X-ray, la utoaji dawa, la kufulia nguo na la utawala.
“Serikali imeelekeza ujenzi huu ufanyike kwa kutumia njia ya manunuzi inayoitwa ‘Force Account’ ambapo Halmashauri inanunua vifaa vya ujenzi na kuajiri mafundi wa kujenga majengo yaliyoelekezwa wakisimamiwa na wataalam wa halmashauri na kamati mbalimbali,” alisema.
Akizungumza na wakazi waliojitokeza kumsikiliza hospitalini hapo, Waziri Mkuu aliwapongeza viongozi wa Halmashauri hiyo kwa kusimamia vizuri ujenzi na kwa kuamua kutumia force account ambayo alisema inapunguza sana gharama za manunuzi.
Aliitaka Halmashauri hiyo isisubiri hadi kazi ya ujenzi ikamilike, na badala yake wahusika wajipange na kuanza kufanya usafi wa eneo linalozunguka hospitali hiyo. “Halmashauri tusikae tu kusubiri ujenzi uishe. Tufanye usafi kuzunguka eneo lote, tupande miti na maua ili mandhari ianze kupendeza,” alisema.
Kuhusu muda wa kukamilisha kazi hiyo, Waziri Mkuu aliwashauri mafundi wazidishiwe muda wa kufanya kazi. “Badala ya kufanya kazi mchana peke yake, bora waongezewe muda wafanye hadi usiku ili kufidia muda uliopotea, na uliobakia ni mfupi mno,” alisema.
Alisema anaamini kazi hiyo itakamilika ndani ya muda mfupi ili huduma zianze kutolewa hapohapo Ruangwa na kuwapunguzia wananchi adha ya kwenda hadi hospitali ya Ndanda.