Home Mchanganyiko MHAGAMA AFUNGUA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI NA USIMAMIZI WA BIASHARA KWA VIJANA...

MHAGAMA AFUNGUA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI NA USIMAMIZI WA BIASHARA KWA VIJANA JIJINI DODOMA

0

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Mhe Jenista Mhagama,akizungumza wakati wa kufungua mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara kwa vijana leo jijini Dodoma ambapo amewataka kuwa wabunifu pamoja na kuitumikia nchi yao kwa uzalendo.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana Ajira na Walemavu, Andrew Massawe,akizungumza na washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara kwa vijana leo jijini Dodoma .

Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Mhe Anthony Mavunde,akizungumza na wadau pamoja na washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara kwa vijana leo jijini Dodoma .

Naibu Waziri ,Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia watu wenyeulemavu,Mhe.Stella Ikupa,akisisitiza jambo kwa wa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara kwa vijana leo jijini Dodoma .

Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara kwa vijana yaliyofanyika leo jijini Dodoma.

Picha na Alex Sonna-Fullshangweblog

…………………

Na.Alex Sonna,Dodoma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu, Mhe Jenista Mhagama amefungua mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa biashara kwa vijana na kuwataka kuwa wabunifu pamoja na kuitumikia nchi yao kwa uzalendo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo jijini Dodoma, Waziri Jenista amesema Serikali imejipanga katika kufanikisha inatoa kipaumbele kwa vijana nchini ikiwemo kutunga Sera rafiki zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi katika ujasiriamali bila kusubiri kujitegemea.

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwezesha na kuboresha mbinu za uendeshaji na usimamizi wa biashara pamoja na urasimishaji wa shughuli za uzalimishaji zinazofanywa na vijana.

” Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wetu mpendwa Dk John Magufuli inalenga kuwawezesha vijana wanaomiliki biashara katika Mikoa husika kukuza na kurasimisha biashara zao ili kuongeza ajira kwa vijana wenzao na watanzania kwa ujumla pamoja na kuchangia pato la Taifa.

” Lakini pia Serikali imepanga kuwaunganisha vijana na fursa za mitaji na mitandao ya huduma za biashara ikiwemo urasimishaji,” amesema Waziri Jenista.

Aidha Mhe Jenista amewataka vijana kuepuka kukaa vijiweni na kuwa watu wanaolalamika bila ilihali Serikali ya Rais Magufuli imekua ikitoa mikopo isiyo na riba katika Halmashauri zake nchini.

” Niwaombe vijana muamke maana nyie ndio mnapaswa kuwa uti wa mgongo katika kuufikia uchumi wa kati. Hampaswi kulalamika, mna nguvu na wengine mna taaluma zenu, tuzitumie kuhakikisha tunaikomboa jamii yetu, sisi kama Serikali tunaahidi kuwaunga mkono na kuwatengenezea mazingira rafiki ya kuwawezesha kufanya biashara zenu bila kusumbuliwa na mtu,” amesema Mhe Jenista.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Mhe Anthony Mavunde amewataka vijana kuamka na kufanya kazi kwa bidii huku wakiamini wanaweza kufikia malengo na ndoto zao bila kikwazo chochote.

” Ondoeni dhana ya kushindwa katika akili zenu, ukiwa kijana unapaswa kufikiri chanya muda wote, Kama hutoamua kujituma na kufanya kazi kwa bidii huku ukiamini unaweza kufanikiwa basi hata aje nani kukwambia utafanikiwa huwezi kumuelewa. Kama vijana ni wakati wa kuamka kwa ari kubwa na kushinda, ” amesema Mhe Mavunde.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana Ajira na Walemavu, Andrew Massawe amesema dira ya Serikali ya awamu ya tano ni kuipeleka Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ambayo itakua chachu ya kukuza pato la Taifa.

” Ili kufikia azma ya uchumi wa kati vijana ndio nguzo pekee yenye mchango mkubwa wa kufanikisha maono ya Serikali. Hivyo Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) wanaendesha mafunzo ya uwezeshaji kwa vijana ili kutengeneza tija katika shughuli za uzalimishaji wanazozifanya kila siku,” amesema Bw Massawe.

Nae Katibu Mtendaji wa NEEC, Bi Beng’i Issa amesema mafunzo hayo yatawafikia moja kwa moja vijana wasiopungua 4000 katika Mikoa yote ya Tanzania bara lakini matokeo yake yanaweza kuwa zaidi ya namba hiyo kutokana na ajira mpya zitakazoibuliwa sambamba na uanzishwaji wa biashara nyingine.