Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akitoa hotuba katika hafla ya kuwaaga wafanyakazi 18 wa kichina waliokuwa katika Mradi wa awamu ya Pili ya Upimaji na utibabu wa Maradhi ya Shingo ya Kizazi hafla iliofanyika Katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazi mmoja Zanzibar.
Meneja wa kitengo cha maradhi yasioambukiza Omar Mwalim Omar akizungumza katika hafla ya kuwaaga wafanyakazi 18 wa kichina waliokuwa katika Mradi wa awamu ya Pili ya Upimaji na utibabu wa Maradhi ya Shingo ya Kizazi hafla iliofanyika Katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazi mmoja Zanzibar.
Mgeni Rasmi Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma akitoa hotuba kuhusiana na maradhi ya shingo ya kizazi katika hafla ya kuwaaga wafanyakazi 18 wa kichina waliokuwa katika Mradi wa awamu ya Pili ya Upimaji na utibabu wa Maradhi ya Shingo ya Kizazi hafla iliofanyika Katika ukumbi wa Wizara ya Afya Mnazi mmoja Zanzibar.
******
Na Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar 28/07/2019
Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed amesema Uchunguzi wa Saratani ya Shingo ya Kizazi kwa Zanzibar umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kugundua maradhi mbali mbali ya akinamama na kupatiwa tiba
Amesema wananchi wengi walijitokeza na kufanyiwa uchunguzi huo na baadhi waliweza kugunduliwa na tatizo hilo.
Hayo aliyasema wakati wa kuwaanga na kuwatunuku vyeti Timu ya Madaktari kutoka jimbo la Jiangsu nchini China pamoja na Madaktari na Wauguzi wa ndani ambao wamemaliza mradi wa awamu ya pili wa kutoa huduma ya upimaji wa saratani ya shingo ya kizazi Zanzibar.
Amesema wananchi waliofanyiwa uchunguzi katika zoezi hilo jumla ya watu 5181 walichunguzwa wagonjwa 72 wamegunduliwa wako katika saratani ya hatua ya awali 15 hatua ya kiwango cha juu ambao wametakiwa wapelekwe ocean road kwa kupatiwa mionzi na wagonjwa saba wamefanyiwa upasuaji na 27 wanahitaji kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya mnazi mmoja .
Waziri huyo alisema kupima afya ni jambo la muhimu kwa kila mmoja wetu kwani kunasaidia kugundulika kwa maradhi mapema na kupatiwa tiba na kupona kwa haraka .
Aidha alisema saratani ya shingo ya kizazi Tanzania inaongoza kuwa na idadi kubwa katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki takwimu zinaonyesha kati ya watu elfu 35 hupata kensa ya shingo ya kizazi kwa kila mwaka kati ya hao asilimia 20 tu ndio hufika hospitali na kupatiwa matibabu.
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mgeni Hassan Juma amewataka wananchi kuzitumia fursa zinazotolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za uchunguzi wa afya katika maradhi mbali mbali ambayo zinatolewa na wataalamu katika Hospitali ya Rufaa Mnazi mmoja .
“Tunatakiwa kufanya uchunguzi wa kiafya hasa sisi akinamama tujichunguze saratani ya matiti ,chingo ya kizazi na hata Tenzi dume kwa akinababa ili tuweze kujigundua matatizo mapema kuliko maradhi mgonjwa yeshamuathiri “alisema Naibu Spika
Naibu huyo amesema anaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwaletea huduma ya matibabu kwa lengo la kufanikisha Taifa lenye wananchi wenye afya bora .
Naibu Spika aliitaka timu hiyo kuendelee kutoa misaada yao ya huduma za kiafya kwa Serikali ya Zanzibar ili kuweza kuwapatia wafanyakazi wa afya ujuzi wa kitaalamu wa kuweza kutoa huduma iliyobora kwa wananchi wao .
Nae Mkuu wa Kitengo cha Maradhi Yasiyoambukiza Omar Mwalim amesema shughuli za upimaji zimekwenda vizuri na madaktari na wauguzi wameweza kuengeza ujuzi wa kazi zao na kufikia malengo yaliyohitajiwa.
Aliitaka Wizara ya Afya kuvungua kitengo maalum cha uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi ii kuweza kupungua tatizo hili na kuondoka kabisa .
Kwa upande wa Mratibu wa Madaktari kutoka China Jasmine Qi Xiaomin alisema uchunguzi wa maradhi ya saratani ya kizazi kutasaidia kuwafanya akinamama wawe na afya bora na kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa .
Pia aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya kwa mapokezi mazuri katika muda wote wa mwezi mmoja wa kutoa huduma kwa wananchi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja .