Naibu Waziri wa Kilimo,akizungumza na wakulima wa pamba juzi wilayani Kwimba.Kulia ni Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Salum Kalli na kushoto ni Mbunge wa Kwimba Shanif Mansoor.
……………………
NA BALTAZAR MASHAKA, KWIMBA
SERIKALI imewatoa hofu wakulima wa zao la pamba na kuwataka wasirubuniwe na walaghai, wapeleke pamba yao sokoni kwani fedha zipo, watalipwa na hakuna mkulima atadhulumiwa.
Pia imewahakikishia wanunuzi wa pamba kuwa hawatapata hasara baada ya serikali kuridhia kutoa ruzuku ya kuwafidia endapo bei ya pamba haitapanda kwenye soko la dunia ifikapo Agosti 15, mwaka huu.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu wa Waziri wa Kilimo Omari Mkumba alipozungumza na wakulima wa vijiji vya wilaya za Magu na Kwimba na baadhi ya wanunuzi wa pamba kwenye wilaya hizo juzi kwa nyakati tofauti.
Mkumba ambaye aliambatana na Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza Salum Kalli alisema kutokana na mdodoro wa bei ya pamba kwenye soko la dunia, msimamo wa serikali wakulima wauze pamba yao kwa bei dira ya sh. 1,200 kwa kilo na si vinginevyo.
Alisema imekubaliana na wanunuzi wanunue kwa bei hiyo na waichambue na kuihifadhi kisha waiuze kwa bei ya itakayokuwa sokoni lakini ikifika Agosti 15 mwaka huu, haijapanda wauze pamba yao na endapo wataiuza pungufu ya senti 69.4 USD serikali itawafidia.
“Licha ya wanunuzi kusuasua kutokana na mdororo wa bei na fedha zilizopo kutokidhi mahitaji ya mzigo uliopo sokoni, msirubiniwe kuwa pamba haina soko la hasha.Kilo ni sh. 1,200 na tunataka wakulima wapate tija kwa sababu wanatumia nguvu nyingi kulima pamba hadi wavune,”alisema Mkumba.
Alieleza kuwa awali wanunuzi walisita kununua pamba kutokana na changamoto ya bei kubwa kulingana na mikataba waliyoingia na wanunuzi wakubwa hivyo waliona wanapata hasara.
Naibu waziri huyo alisema malalamiko ya wakulima kuwa hakuna fedha baada ya kuuza pamba yao yalitokana na benki kugoma kuwakopesha wanunuzi zikihofia kuzamisha fedha za watanzania, lakini serikali ilipoingilia kati zimeamua kuwakopesha wafanyabiashara ili waingie sokoni.
“Wanunuzi walikuwa hawana uhakika wa biashara na mitaji yao.Sasa serikali imebeba dhamana hiyo na yote hayo ni kumjali mkulima.Hivyo wakulima mnapaswa kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa kuchapa kazi kwa ajili ya maendeleo ambayo hayaji bila kufanya kazi,”alisema Mkumba.
Pia aliwasisitiza wakulimakulipa madeni ya pembejeo ili mwakani waondokane na uhaba wa viaududu na mbegu ili walime kwa tija zaidi na kujiongezea kipato na kubadilisha maisha yao kiuchumi.
Aidha, Katibu wa CCM, Kalli alisema Rais Magufuli analala na kuamka na shida za wananchi na kuwataka wakulima wasikubali kubabaishwa na kurubuniwa na wadanganyifu kwani serikali imewadhamini wanunuzi wa pamba licha ya bei kushuka kwenye soko.
“Wapo wapo vishoka waliingia kuwatisha wakulima kuwa pamba Mwanza ni siasa ili wauze kwa bei chee, lakini serikali imeingilia jambo hili kuwanusuru wakulima kwa kulipa fidia endapo watauza pamba kwenye soko chini ya senti Dola 68.Tuwatie shime wanunuzi wapate idea ya serikali waingie sokoni,”alisema Kalli.
Naye Mbunge wa Kwimba Shanif Mansoor alisema serikali kutoa ni faraja kwa wakulima baada ya serikali kutoa ruzuku kwenye pamba kwani kwa mara ya kwanza hiyo ni historia na ni vizuri wakulima wakaelezwa ili wanununuzi wasiwaonee.
“Nimefarijika kuona Serikali ya Rais John Magufuli ikitoa ruzuku kwenye pamba, wanunuzi watapata fidia na hakuna hasara na nadhani wataingia sokoni baada ya benki kukubali kutoa fedha.Lakini wanunuzi nao watoe bei halali,”alisema Mbunge huyo wa Kwimba