Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Bw. Timoth Anderson alitoa maelezo kwa wageni waliotembelea banda la TEWW, juu ya sifa za kujiunga na Taasisi katika programu za Shahada, Stashahada na Astashahada , Katika Maonesho ya Vyuo vikuu Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam. Maonesho hayo yanafanyika toka 15-20 Julai 2019
Afisa Udahili wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Bw. Justine Mbwambo
akisisitiza jambo kwa mgeni alietembela banda la TEWW katika maonesho ya Vyuo
Vikuu ambayo yanaendelea kufanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Mtumishi toka TEWW Bi. Felister Lyimo (Kulia) akitoa ufafanuzi juu ya ujazaji wa
fomu ya kujiunga na na TEWW, kwa mgeni alietembelea banda la Taasisi ya Elimu ya
Watu Wazima, katika Maonesho ya Vyuo Vikuu yanayoendelea kufanyika katika
viwanja vya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Idara ya Elimu kwa Umma na Shule Huria Bw. Placid Balige akiongea na
waandishi wa habari (hawapo pichani) juu ya namna ambavyo Taasisi ya Elimu ya
Watu Wazima (TEWW) inatekeleza mkakati wa kuwawezesha vijana wa Kitanzania waliokosa elimu kupata Stadi za kazi, stadi za maisha na ujuzi wa Ujasiriamali ili kuwezesha Tanzania ya Viwanda kufikiwa.
***************
Na Timoth Anderson – TEWW
Taasisi ya elimu ya watu wazima (TEWW) imesema imeweka mkakati wa masomo wa kitaifa ambao utakwenda sambamba na Mpango Changamani kwa Vijana Walio Nje ya mfumo Rasmi wa Elimu maarufu kama ‘IPOSA’ ili kuwafikia Vijana wa kike na wa kiume ambao hawajawahi kwenda shule, wanafunzi walioacha shule za msingi, wanafunzi waliomaliza darasa la saba lakini hawajapata fursa ya kuendelea, wanafunzi waliohitimu masomo yao kupitia program ya MEMKWA, Wasichana walioacha shule kwa changamoto mbalimbali kama vile ujauzito na ndoa za utotoni Kauli hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Idara ya Elimu kwa Umma Shule Huria, Bw. Placid Balige wakati alikuwa akizungumza na waandishi habari kwenye maonesho ya 14 ya Vyuo vya elimu ya juu sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika viwanja vya mnazi mmoja.
“Taarifa ya tathmin ya Mpango wa Elimu Changamani baada ya msingi (MECHAM) ya mwaka 2015,Utafiti uliofanywa na Wizara ya Elimu, Sayansi ya Teknolojia wa mwaka 2015 na taarifa ya takwimu ya Elimu ya msingi zinaonesha watoto wa kati ya miaka 14-17 wapatao 2,256,940 hawapo shule japokuwa ilibidi wawepo shule hivyo TEWW, Wizara yetu, wakaanza kuandaa mpango ambao hapana mtoto atakaeachwa kupewa elimu”.Amesema Balige.
Ameongeza kuwa, watoto walioingia katika ndoa na mimba za utotoni na kukatisha masomo yao wamepata mafanikio makubwa kwani TEWW kupitia miradi yake mbalimbali wamewafundisha stadi za maisha jambo lililopelekea kuwawezesha kujiajiri wenyewe hali ambayo itawawezesha wale wenye nia ya kurudi shuleni kwa mfumo rasmi kurudi kwakuwa wameshapewa stadi za maisha juu ya kukabiliana na mazingira yao.
Aidha, Bw. Balige ameongeza kuwa , watoto hao wameweza kufungua maduka na
kuweza kudhalisha bidhaa zao wenyewe ikiwemo kutengeneza sabuni, kusindika
chakula jambo lililopelekea kupata mkopo wa asilimia 4 wa vijana unaotolewa na
Halmashauri katika maeneo yao ili kuwakomboa vijana kiuchumi.
“Tumeweza kuwafikia vijana 3000 katika mkoa wa Dodoma,Rukwa na Lindi ambao walipata ndoa za utotoni na kukatisha masomo yao kwa sasa wameweza hata kujiunga Vikundi na kuweza kupata mkopo wa Manispaa wa asilimia 10 unatolewa nchi nzima”. Amesema Balige.
Aidha amesema, Taasisi hiyo ilianzishwa na Sheria ya Bunge Namba 12 ya Mwaka 1975 ambapo pamoja na majukumu mengine inatoa Mafunzo kuanzia ngazi ya Astashahada, Stashahada na Shahada katika eneo la Elimu ya Watu Wazima na Mafunzo Endelevu pamoja na Ustawi wa jamii kwa njia ya ana kwa ana na kwa njia ya masafa ili kuwaandaa wataalamu wa Elimu ya Watu Wazima hiyo ikiwa ni mtekelezaji wa Ilani ya chama cha Mapinduzi na kwasababu ni mpango mahususi katika kuchagiza Tanzania ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.