Tabia ya Wakandarasi kuchelewa kukabidhi kazi kwa wakati na kwa ubora haitakubalika kwenye miradi ya ujenzi ya Serikali.
Hayo yamebainishwa na Afisa Tarafa Mihambwe Ndugu Emmanuel Shilatu wakati alipotembelea kufuatilia maendeleo ya miradi ya ujenzi wa umaliziwaji wa maboma ya Madarasa kufuatia Serikali kutoa fedha za kukamilisha ujenzi huo na kuweka na Madawati.
Akizungumza na Mwandishi wetu, Gavana Shilatu alisisitiza uzembe wowote wa kukabidhi kazi kwa wakati na kwa ubora hautavumilika.
“Kwanza kabisa tunamshukuru Rais Magufuli kutoa fedha za kumalizia maboma nchi nzima. Kila nilipopita kwenye miradi ya shule zote nimewasisitiza Wakandarasi kuheshimu mkataba, kuheshimu BOQ, kuzingatia ubora unaoendana na thamani ya pesa. Nimewaambia ndani ya siku 5 kuanzia sasa miradi yote iwe imekamilika ipasavyo, nitaenda tena kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yangu yote niliyoyatoa.” alisisitiza Gavana Shilatu.
Tarafa ya Mihambwe imebahatika kupata fedha Tsh. Milioni 42.5 kukamilisha maboma ya madarasa matatu yaliyopo shule za Msingi za Misufini, Mmalala na Ngongolo.