**************
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. January Makamba amewahakikishia wananchi kuwa bei ya mifuko mbadala itaendelea kushuka.
Mhe. Makamba amesema hayo wakati akizungumzia tathmini ya kampeni ya katazo la mifuko ya plastiki lililoanza kutekelezwa na Serikali hapa nchini Juni mosi 2019.
Amesema hivi sasa viwanda vingi vinaendelea kuagiza mitambo ya kutengeneza mifuko mbadala na kuwa hadi kufikia Septemba mwaka huu bei itakuwa imeshuka na ubora wa mifuko hiyo utaongezeka.
Waziri Makamba alibainisha kuwa changamoto iliyojitokeza ni kwamba zuio la mifuko ya plastiki liliahirishwa mara kwa mara kwani lilishatangazwa siku za nyuma hivyo wawekezaji wa mifuko mbadala walidhani safari hii lingeahirishwa tena hivyo kupelekea kutoagiza mitambo ya kuzalisha mifuko mbadala kwa wakati.
Itakumbukwa kuanzia mwaka 2010 hadi 2019 Serikali imekuwa ikikutana na wadau ili kujenga uelewa na kukusanya maoni kuhusu nia ya kupiga marufuku mifuko ya plastiki.
Mhe. Makamba alifafanua kuwa moja ya kazi kubwa ilikuwa ni kuwashawishi tena wawekezaji na wafanyabishara wa mifuko mbadala kuwa safari hii Serikali imeamua kwa dhati kutekeleza katazo la mifuko ya plastiki.
“Hivi tunavyoongea tayari wenye viwanda na wafanyabishara wameshtuka na kutumia fursa hii kuingiza mitambo na kuzalisha kwa wingi mifuko mbadala,” alisema.
Akizungumzia kuhusu malalamiko ya ukubwa wa bei ya mifuko mbadala kutoka kwa wananchi alisema zamani ile mifuko ya plastiki si kweli ilikuwa inatolewa bure unaponunua bidhaa bali ilikuwa inajumuishwa na bei ya bidhaa yenyewe.
“Unajua watu wanasahau kuwa katika mifuko ya rambo kulikuwa na gharama ya uzalisha lakini bei yake iliingizwa kwenye bidhaa na bei yake ilikuwa ni shilingi hamsini na mia lakini mtu hakwambii, unaenda kununua unga anakwambia ni bure lakini sasa hivi wameamua kutenganisha na watu wanaona bei ni kubwa,” alisema.
Aliongeza kuwa unapoleta mabadiliko ni lazima uzungumze na wadau na wananchi wayaone mabadiliko unayotaka kuleta kuwa yana manufaa kwao na hawawezi kuyapinga.
Alisema watu wanapinga mabadiliko kama hawana uhakika kama yatawasaidia, sisi tuliyochofanya ni kuwashawaishi kuyapokea mabadiliko yenye manufaa kwao.
Wakati wa utekelezaji wa katazo hilo kumekuwa na changamoto ya bei ya mifuko mbadala kuwa kubwa ambapo mifuko ya non- woven inauzwa kati ya sh. 300 hadi 1500.
Hata hivyo, Waziri Makamba ameuhakikishia umma wa watanzania kuwa mwenendo wa bei ya mifuko mbadala utaendelea kushuka siku hadi siku