Wanafunzi wasichana kutoka Shule mbalimbali wilaya ya Arumeru wakifatilia mada wakati Wiki ya Nelson Mandela inayolenga kuwahamasisha kusoma masomo ya Sayansi na Uandisi. |
Na Mwandishi Wetu,Arusha
Balozi wa Afrika Kusini nchini,Thami Mseleku ameitaka jamii kuwaendeleza wasichana katika masomo ya sayansi kutokana na mchango wake katika kutatua changamoto zinazoikabili jamii.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Nelson Mandela katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela(NM-AIST) mkoani hapa alisema mila na desturi za kuona wavulana pekee ndio wanaopaswa kuwa wanasayansi imepitwa na wakati.
“Jamii kwa ujumla wake inapaswa kuona umuhimu wa kuwapa elimu wasichana kufanya hivyo ni kuwatengenezea maisha yao katika siku zijazo jambo ambalo Hayati Nelson Mandela alilipa kipaumbele,unapompa elimu msichana unakua umeelimisha jamii nzima,”alisema Balozi Mseleku
Naibu Makamu Mkuu wa NM-AIST,Taaluma,Utafiti na Ubunifu,Profesa Anthony Mshandeti alisema uongozi wa Chuo hicho unaadhimisha kwa mwaka wa tano kwaajili ya kuhamaisha masomo ya sayansi na teknolojia kutoa mchango katika kuchangia uchumi wa viwanda.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo hicho,Dk Lilian Passape alisema wiki ya maendeleo itahusisha mambo mbalimbali kwaajili ya wanafunzi wa shule za sekondari,wajasiriamali wanaokutanishwa na taasisi za fedha, maonesho ya ubunifu na kuwatembelea wagonjwa katika hospitali ya Mount Meru.
Alisema watatumia maadhimisho hayo kugharamia wananchi kupimwa Homa ya Ini na ambao hawatutwa na vimelea vya ugonjwa huo watapewa chanjo na ambao watakutwa nao wataunganishwa na hospitali ya Mount Meru kwaajili ya kuendelea na matibabu zaidi.