Home Mchanganyiko LUGOLA: POLISI VITAVISHUGULIKIA VYAMA VYA SIASA VITAKAVYOSHAWISHI WANANCHI KUVURUGA UCHAGUZI SERIKALI ZA...

LUGOLA: POLISI VITAVISHUGULIKIA VYAMA VYA SIASA VITAKAVYOSHAWISHI WANANCHI KUVURUGA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

0

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Mji wa Kibara, Jimboni kwake Mwibara, Bunda, leo. Lugola amesema Jeshi la Polisi litahakikisha linawashughulikia wanasiasa watakaojaribu kuwashawishi wananchi kufanya fujo kwa lengo la kuvuruga uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini mwezi oktoba, 2019.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto), akiwasili Ofisi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara, leo, kwa ajili ya kwenda kuwasalimia wanaCCM wilayani humo, kabla ya kuanza ziara yake ya kuzungumza na wananchi jimboni kwake Mwibara.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, (wapili kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, Isack Maela, wakati alipokua anatoa maelezo mafupi kabla ya kumkaribisha Waziri huyo kuzungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Mji wa Kibara, Jimboni kwake Mwibara, leo. Katika hotuba yake kwa wananchi hao, Lugola amesema Jeshi la Polisi litahakikisha linawashughulikia wanasiasa watakaojaribu kuwashawishi wananchi kufanya fujo kwa lengo la kuvuruga uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini mwezi oktoba, 2019. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

………………….

Na Felix Mwagara, Mwibara (MOHA)

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema Jeshi la Polisi litahakikisha linawashughulikia wanasiasa watakaojaribu kuwashawishi wananchi kufanya fujo kwa lengo la kuvuruga uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Lugola alisisitiza kuwa, kisitokee chama chochote cha siasa kitakachojaribu kuvuruga uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwezi oktoba mwaka huu 2019, ambao Watanzania wengi wamejipanga kufanya uchaguzi huo kwa amani na utulivu.

Lugola ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara alipokuwa anazungumza na wananchi wa Mji wa Kibara, Jimbo la Mwibara, Wilaya ya Bunda, Mkoani Mara, leo, ambapo amesema wananchi wajiepushe kudanganywa au kutumbukia katika mtego wowote wa wanasiasa.

“Wizara yangu kupitia Jeshi la Polisi haita kuwa tayari kuona na kumuacha raia wa Tanzania au asiye raia akijihusisha na vitendo vya kuhujumu uchaguzi au kuleta fujo, atadhibitiwa bila kujali nafasi yake, au uwezo wake kiuchumi, hii Serikali siyo ya kuchezewa, hivyo natuma salamu kama mlikuwa na mawazo hayo yaondoeni, hatutamuonea mtu huruma ambaye analengo la kuvuruga amani yetu,” alisema Lugola.

Pia Waziri Lugola alivitaka vyama hivyo viwe na uzalendo na nchi yao na pia viwe na hitikadi na malengo ya kisiasa ambayo hayaleti fujo kwa kufuata sheria za nchi.

Aidha, Lugola kwa mara nyingine alizungumzia uhalifu katika ziwa Victoria, akiwataka Polisi waongeze kasi kwa kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo hayo ya ziwa kwa lengo la kudhibiti uhalifu huo.

“Huu uhalifu katika ziwa Victoria utashughulikiwa, hii ni awamu ya tano ambayo inaongozwa na Rais Dkt John Magufuli, hivyo tunataka wananchi muishi katika nchi yenu kwa amani na utulivu,” alisema Lugola.

Waziri Lugola anaendelea na ziara jimboni kwake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kufanya mikutano ya hadhara akisikiliza kero za wananchi jimboni humo, na pia kuiongoza ligi yake, Kangi Bomba ambayo inashirikisha wananchi jimboni humo kufanya mashindano ya mpira wa miguu, pete, pamoja na michezo mbalimbali.