Home Mchanganyiko WATANZANIA WAHAMASISHWA KUTEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII NCHINI ILI KUKUZA UTALII WA NDANI

WATANZANIA WAHAMASISHWA KUTEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII NCHINI ILI KUKUZA UTALII WA NDANI

0

Chama cha Walimu (CWT) Jiji la Dodoma kimewataka Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya Utalii ili kukuza Utalii wa ndani hapa nchini Tanzania katika kumuunga Mkono Rais Dr John Pombe Joseph Magufuli kwenye azma yake ya kuhakikisha sekta ya Utalii inakua na kuchangia kwa asilimia kubwa kwenye pato la Taifa na kuliingizia Taifa fedha nyingi za kigeni.

Hayo yamesemwa jana na Katibu wa CWT Wilaya ya Dodoma Mjini Ndg Kelvin Mahundi kwa niaba ya walimu wenzake wakati wa ziara fupi ya Mafunzo katika Kituo cha Mali kale cha Michoro ya Miambani,Kolo Wilayani Kondoa-Dodoma ambapo walimu hao kwa umoja wao walimshukuru Mbunge Mavunde kwa kugharamia ziara yao Kufika hapo Kolo na kuutaka umma wa watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vya Utalii hapa nchini na hivyo kujifunza masuala ya hifadhi,historia na utamaduni wa jamii mbalimbali.

Katika ziara hiyo ya Mafunzo Walimu hao wa Shule za Msingi na Sekondari Jijini Dodoma waliongozana na Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh Anthony Mavunde  ambaye pia aliungana na walimu hao kutoa wito kwa Jamii ya Watanzania kujiwekea utaratibu wa kutembelea vivutio vya Utalii kama ambavyo yeye aliona umuhimu wa kuwapeleka walimu wa Jiji la Dodoma kwenda kujifunza mambo ya Mali kale katika Michoro ya miambani-Kolo Kondoa.

“Hapa Kolo,Kondoa ni eneo zuri la kujifunza kuhusu historia na utamaduni wa jamii ya watu wanaoishi eneo hili kupitia hapa Kituoni.Awamu ya kwanza niliamua kuwaleta walimu na awamu ya pili sasa nitawaleta wanafunzi ili waje wajifunze nao pia.Nitaendelea kuwa Balozi mzuri katika kuhamasisha watu waje waone urithi huu wa Dunia kupitia michoro ya kwenye miamba hapa Kolo-Kondoa”Alisema Mavunde

Akitoa maelezo ya awali msimamizi wa kituo hicho Ndg Zuberi Mabie amesema kwamba hivi sasa idadi ya watu wanaofika hapo inazidi kuongezeka kila mwaka hasa baada ya kukamilika kwa miundombinu ya barabara ya Babati-Dodoma ambayo imerahisisha sana kufikika kwa eneo hilo na hivyo kuendelea kutoa rai kwa Watanzania kuwa mstari wa mbele kutembelea kituo hicho kujifunza kuhusu michoro na utamaduni wa jamii husika.