Home Michezo KUNAMBI AMTANGAZA MBWANA MAKATA KUINOA DODOMA FC

KUNAMBI AMTANGAZA MBWANA MAKATA KUINOA DODOMA FC

0

Na.Alex Sonna,Dodoma

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Godwin Kunambi amemtambulisha aliyekua kocha wa zamani wa Polisi Tanzania, Mbwana Makata kuwa Kocha Mkuu wa Dodoma FC.

Kunambi amesema wao kama Jiji la Dodoma wamejipanga kuhakikisha Timu hiyo inapanda daraja kwenda Ligi Kuu ili kuhakikisha wanampa heshima Rais Dk John Magufuli kwa kuipa Dodoma hadhi ya Jiji.

” Ni lazima tumpe heshima Rais wetu Dk John Magufuli kwa kutupa hadhi ya Makao makuu, kutujengea uwanja wa kimataifa wa ukubwa wa kubeba watu zaidi ya Laki Moja, hivyo ni lazima tuwe na timu imara ambayo itakua Ligi Kuu.

” Lengo letu ni kupanda daraja kutoka Ligi daraja la kwanza kwenda Ligi Kuu, tutampa ushirikiano kocha Makata katika usajili, mchezaji yeyote ambaye atamhitaji sisi tutakua tayari kutoa pesa ili asajiliwe,” amesema Kunambi.

Nae Meya wa Jiji hilo Profesa Davis Mwamfupe amewataka wanasiasa kutoiingilia Timu hiyo na kumuahidi ushirikiano kocha Makata huku akimtaka kufanya kazi kubwa ya kuhakikisha Dodoma FC inapanda Ligi Kuu.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum, Mhe Felista Mabula amesema uwezo uliooneshwa na Kocha Makata akiwa anainoa Polisi Tanzania ni mkubwa hivyo wanaamini ataendeleza ubora wake akiwa na Dodoma FC ili iweze kupanda Ligi Kuu.

Akizungumza baada ya kutambulishwa Kocha Makata ameahidi kuhakikisha anatimiza malengo aliyowekea na uongozi wa Timu hiyo kwa kuipandisha Dodoma FC Ligi Kuu Tanzania.