Home Michezo YANGA YASAJILI MRITHI WA GARDIEL MBAGA

YANGA YASAJILI MRITHI WA GARDIEL MBAGA

0

Na Mwandishi Wetu,
KLABU ya Yanga SC imefanikiwa kumsajili beki wa kushoto, Muharami Salum Issa ‘Marcelo’ kutoka klabu ya Malindi ya kwao, Zanzibar.
Lakini Yanga imelazimika kufanya mazungumzo ya kiungwana na wapinzani wao wa Tanzania Bara, Singida United ili wawaachie mchezaji huyo ambaye tayari alikuwa amekwishamalizana na klabu hiyo na kutangazwa.
Ni kama ilivyokuwa kwa kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ msimu uliopita ambaye naye alianza kusajiliwa na Singida United kutoka JKU ya Zanzibar, lakini akahamia Yanga SC.
Na hiyo ni kwa sababu Rais wa klabu ya Singida United, Dk Mwigulu Nchemba (Mbunge) ni mwanachama na mpenzi mkubwa wa klabu ya Yanga.

Marcelo anasajiliwa kuziba pengo la Gardiel Michael Mbaga aliyegoma kusaini mkataba mpya na taarifa zinasema kwamba anajiunga na Bidvest Wits ya Afrika Kusini, huku watani wa jadi, Simba SC ya Dar es Salaam wakimuwania.
Marcelo anakuwa mchezaji mpya 13 kusajiliwa na Yanga SC na wa tano tu mzawa, baada ya mabeki Ally Mtoni ‘Sonso’ kutoka Lipuli FC, Ally Ally kutoka KMC ya Kinondoni, viungo wa ulinzi, Abdulaziz Makame kutoka Mafunzo ya Zanzibar na Mapinduzi Balama kutoka Alliance FC ya Mwanza,
Wengine saba wote wa kigeni ambao ni kipa Farouk Shikalo kutika Bandari ya kwao, Kenya, Sadney Urikhob kutoka Namibia, Lamine Moro kutoka Ghana, Juma Balinya kutoka Uganda, Issa Bigirimana, Patrick Sibomana wote wa Rwanda, Mustapha Seleman kutoka Burundi na Maybin Kalengo kutoka Zambia.