Home Mchanganyiko VETA KUSHIRIKIANA NA AIRTEL KULETA MFUMO WA UFUNDISHAJI KUPITIA INTERNET

VETA KUSHIRIKIANA NA AIRTEL KULETA MFUMO WA UFUNDISHAJI KUPITIA INTERNET

0

Mkurugenzi wa SIDO Bw. Sylvester Mpanduji akiongea katika banda la VETA katika viwanja vya maonesho vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam

Mkurugenzi Mkuu VETA, Dkt. Pancras Bujulu(Wa kwanza kushoto)akiwa pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa rasilimali watu na Utawala Bw. Felix Staki (Katikati)  na anaefuata ni Meneja uhusiano VETA, Bw. Sitta Peter wakiongea jambo katika banda la VETA kwenye viwanja vya maonesho ya biashara vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam

Meneja Mradi wa VSOMO kutoka VETA,Bw.Charles Mapuli akionesha mfano wa mfumo wa Umeme unaotumika majumbani, viwandani pamoja na katika makapuni.

*****************

NA EMMANUEL MBATILO

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) wameamua kuleta mfumo katika jamii huitwao VSOMO ambao utamsaidia mtu ambaye anahitaji kupokea mafuno ya Ufundi Stadi kutumia internet hasa ukiwa na laini ya Airtel.

Ameyasema hayo leo Meneja Mradi wa VSOMO kutoka VETA,Bw.Charles Mapuli katika Maonyesho ya biashara katika viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na Fullshangweblog,Bw.Mapuli amesema kuwa teknolojia hiyo itamfanya mwanafunzi kupata maarifa ya msingi ya awali kwa kujisomea mwenyewe kupitia simu yake na gharama ya ada atatakiwa kulipa kwa kila kozi shilingi 120,000 pia inaweza kulipwa kwa mara moja au kwa awamu mbili, yaani shilingi 60,000 anapoanza mafunzo ya nadharia kwenye simu na kumaliza shilingi 60,000 kabla ya kuanza mafunzo ya vitendo.

“VSOMO inamuwezesha msomaji kupata ujuzi kwa muda mfupi sana zaidi kuongza masaa ya kujifunza kwa siku.Hii maana yake ni kwamba inapunguza muda wa mwanafunzi kukaa VETA ili kujifunza nadharia badala yake kutoa nafasi tu kwaajili ya kufika na kufanya mazoezi kwa vitendo kwani nadharia unajisomea na kufaulu kupitia simu yako”. Amesema Bw.Mapuli.

Ameongeza kuwa wakufunzi wa VETA katika fani mbalimbali ndio wanatumika kutengeneza mafunzo ya nadharia ili kuwezesha usimamizi wa mafunzo kwa vitendo.

Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu VETA, Dkt. Pancras Bujulu amesema kuwa dhumuni la VETA kufika katika maonyesho hayo ni pamoja na kuonyesha mchango wa VETA  katika maendeleo ya Taifa hasahasa katika sekta ya viwanda hivyo jukumu lao ni kuunga mkono mpango wa taifa kwa kauli mbiu ya “usindikizaji wa mazao ya kilimo kwa maendeleo ya Viwanda”.