Home Michezo TAIFA STARS YACHAPWA 3-0 NA ALGERIA NA KURUDI MIKONO MITUPU AFCON 2019

TAIFA STARS YACHAPWA 3-0 NA ALGERIA NA KURUDI MIKONO MITUPU AFCON 2019

0

Na Mwandishi Wetu
TANZANIA imekamilisha ushiriki wake wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 kwa kuchapwa mabao 3-0 usiku wa Jumatatu katika mchezo wa mwisho wa Kundi C Uwanja wa Al Salam mjini Cairo nchini Misri.
Kipigo hicho kinamaanisha Taifa Stars inaondoka Misri bila hata pointi moja, ikishika mkia kwenye kundi hilo, nyuma ya jirani zao, Kenya waliovuna pointi tatu, ingawa nao pia wanarejea nyumbani, huku Senegal iliyomaliza na pointi sita katika nafasi ya pili ikiungana na Algeria iliyokusanya pointi tisa kwenda hatua ya 16 Bora.
Taifa Stars ya kocha Emmanuel Amunike imeshindwa kuvunja rekodi ya kikosi cha mwaka 1980 kilichoshiriki fainali hizo mjini Lagos, Nigeria ambacho angalau kiliambulia pointi moja baada ya sare na Ivory Coast ya 1-1, kikitoka kufungwa 2-1 na Misri na 3-1 na wenyeji, Nigeria.

Katika mchezo wa jana, mabao yaliyoizamisha Taifa Stars yalifungwa na mshambuliaji wa FenerbahceI ya Uturuki, Islam Slimani dakika ya 34 na kiungo wa Napoli ya Italia, Adam Ounas dakika ya 39 na 45 na ushei.
Ikumbukwe mechi mbili za mwanzo, Taifa Stars ilichapwa mabao 2-0 na Senegal na 3-2 na Kenya ikishiriki fainali za AFCON kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39.
Mechi nyingine ya Kundi C jana, Senegal iliichapa Kenya 3-0, mabao ya washambuliaji Ismaila Sarr wa Rennes ya Ufaransa dakika ya 63 na Sadio Mane wa Liverpool ya England dakika za 71 na 78 kwa penalti. Mane angeweza kuondoka na mpira kama mkwaju wake mwingine wa penalti usingepanguliwa na kipa wa  Harambee Stars, Patrick Musotsi Matasi.
Kulikuwa na mechi za Kundi D pia, Ivory Coast ikiichapa Namibia 4-1 na Morocco ikiilaza Afrika Kusini 1-0 hivyo washindi wote kusonga mbele, hatua ya 16 ya michuano hiyo.
Uwanja wa Juni 30 mjini Cairo, mabao ya Tembo wa Ivory Coast yalifungwa na M. Gradel wa Toulouse ya Ufaransa dakika ya 39, Sereso Die wa Basel ya Uswisi dakika ya 58, Zaha wa Crystal Palace  ya England, dakika ya 84 na Gnaly  Maxwell Cornet wa Lyon ya Ufaransa dakika ya 89, wakati la Namibia lilifungwa na kiungo wa Cape Umoya United ya Afrika Kusini, Joslin Kamatuka dakika ya 71.
Na bao pekee la kiungi wa Al Shabab ya Saudi Arabia, Mbark Boussoufa dakika ya 90 Uwanja wa Al Salam mjini Cairo likatosha kuipa Morocco ushindi wa 1-0 dhidi ya Afrika Kusini. Morocco imemaliza kileleni mwa Kundi D kwa pointi zake tisa, ikifuatiwa na Ivory Coast pointi sita, Afrika Kusini pointi tatu wakati Namibia kama Tanzania, 0.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Metacha Mnata, Erasto Nyoni, David Mwantika/Himid Mao dk52, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Ally Mtoni ‘Sonso’, Mudathir Yahya, Feisal Salum/John Bocco dk85, Mbwana Samatta, Simon Msuva na Farid Mussa/Adi Yussuf dk46.
Algeria; Rais M’Bolhi, Rafik Halliche, Mehdi Zeffane, Mehdi Tahrat, Mohamed Fares, Mehdi Abeid/Baghdad Bounedjah dk79, Adam Ounas/Riyad Mahrez dk74, Ismael Bennacer/Adlene Guedioura dk57, Hichem Boudaoui, Islam Slimani na Andy Delort.