Home Mchanganyiko JITIHADA ZA SERIKALI KUPUNGUZA UMASIKINI ZAFANIKIWA

JITIHADA ZA SERIKALI KUPUNGUZA UMASIKINI ZAFANIKIWA

0

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa (kulia), akipeana mkono na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), baada ya  uzinduzi wa Jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), jijini Dodoma.

Muonekano wa Jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Jijini Dodoma, lililozinduliwa na  Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa.

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa (kulia), akimkabidhi  Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,  Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), kitabu cha matokeo ya viashiria muhimu vya utafiti wa mapato na matumizi ya Kaya binafsi kwa Tanzania Bara wa mwaka 2017/18, jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa sita kulia)  na viongozi wengine wakiwa wamenyanyua kitabu cha matokeo ya viashiria muhimu vya utafiti wa mapato na matumizi ya Kaya binafsi kwa Tanzania Bara wa mwaka 2017/18, jijini Dodoma

*******************

Na. Josephine Majura na Peter Haule, WFM, Dodoma

 

Kiwango cha umaskini nchini Tanzania kimepungua kwa asilimia mbili, ikiwa ni matokeo ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano ya kupunguza umasikini kwa wananchi hasa wa hali ya chini.

Hayo yamebainishwa wakati Waziri Mkuu Mhe. Kassimu Majaliwa, akizindua ripoti ya matokeo ya viashiria muhimu vya utafiti wa mapato na matumizi ya mwaka 2017-18 na jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Mkoani Dodoma.

Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa,  amewataka Watakwimu nchini kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo mbalimbali wakati wa kutekeleza majukumu yao hususan kuzalisha  na  kusambaza takwimu zenye viwango vya kitaifa na kimataifa ili kuisaidia Serikali kujua mahitaji yaliyopo.

“Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, inatambua umuhimu wa takwimu zenye ubora, kwa kuwa  ndiyo macho na masikio ya Serikali katika kufuatilia na kutathmini mipango ya maendeleo ya nchi”, alieleza Mhe. Majaliwa.

Mhe. Majaliwa, alisema kuwa takwimu bora hutoa fursa kwa Serikali kufanya mapitio ya sera, mipango na mikakati kulingana na hali ilivyo kwa wakati husika na pia kupima ilikotoka, ilipo na kutabiri inakoelekea hivyo kupima mwenendo wa jitihada za Serikali.

Aidha aliiagiza Ofisi ya Taifa ya Takwimu Nchini (NBS), kuhakikisha Halmashauri zote nchini zinakuwa na Afisa Takwimu ili kurahisisha upatikanaji wa takwimu kwa wakati ili kuweza kusaidia maendeleo nchini.  

Kwa upande wake Naibu wa Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa Wizara yake imepewa jukumu la kusimamia Uchumi wa Taifa, lakini haiwezi kusimamia uchumi bila kuwa na takwimu rasmi na sahihi.

 “Katika kipindi cha takribani miaka mitatu na nusu tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, umaskini nchini umepungua hadi kufikia takribani asilimia 26 kutoka asilimia 28, ikiwa ni sawa na kupungua kwa asilimia mbili”, alisisitiza Dkt. Kijaji.

Dkt. Kijaji alisema kuwa  matokeo ya tafiti yaliyozinduliwa na Mhe. Kassim Majaliwa, yameonesha kupungua kwa umaskini wa watanzania waishio vijijini kwa asilimia 3.1 kati ya mwaka 2011/12 na mwaka 2017/18.

Alieleza kuwa hayo ni matunda ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Kiongozi wake, Mhe. Rais, Dkt. Magufuli.

Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Albina Chuwa, alisema kuwa utafiti wa mwaka 2017/2018 umetumia teknolojia ya kisasa inayojulikana kama Survey Solution ambayo ni tofauti na njia ya awali ya kutumia madodoso yaliyochapishwa hivyo kupunguza gharama za kufanya tafiti za kijamii.

Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa akiwemo Mwakilishi wa Benki ya Dunia Bw. Denis Biseko, wameipongeza Serikali kwa kupunguza kiwango cha umasikini kwa takribani asilimia 2, na pia wamepongeza matokeo ya utafiti huo ambao umezingatia usawa wa kijinsia hivyo kuwa chachu ya maendeleo kwa kuwa ni moja ya lengo la mashirika hayo.