Home Mchanganyiko SIMA-MISITU YA MIKOKO HUSAIDIA KUZUIA MABADILIKO YA TABIANCHI

SIMA-MISITU YA MIKOKO HUSAIDIA KUZUIA MABADILIKO YA TABIANCHI

0

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazingira, Mhe. Mussa Simma amesema misitu ya mikoko husaidia kuzuia mabadiliko ya tabianchi kutokana na joto la dunia.

Mhe. Sima amesema hayo leo Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Chambani, Yussuf Salim Hussein aliyetaka kujua Serikali inafaidikaje na rasilimali ya miti ya kikoko iliyoanza katika Ukanda wa Pwani ya Tanga hadi Mtwara.

Naibu Waziri Sima alisema mfumo wa ikolojia unaopatikana katika misitu ya mikoko unasaidia kuondoa kiwango kikubwa cha hewa ya ukaa ambayo ingeweza kuongeza joto la dunia na kusababisha mabadiliko ya tabianchi.

“Umuhimu wa misitu ya mikoko ni pamoja na kuwa na mazalia na makazi ya viumbe wa baharini na pia misitu hii huhifadhi fukwe na mazingira ya bahari na hivyo kuokoa mali na maisha ya wakazi wa pwani kuepukana na vimbunga, dhoruba na mawimbi ya bahari,” alisema.

Akuendelea kujibu swali hilo Mhe. Sima alisema mikoko husaidia kuchuja udongo, uchafu na sumu inayoweza kutiririshwa na maji na kuingia baharini na kuharibu matumbawe (mawe laini yanayopatikana baharini) ambayo ni makazi ya samaki.

Aidha, aliongeza kuwa misitu ya mikoko ni muhimu kwa Taifa kwani husaidia katika malighafi ya ujenzi yaani mbao, ufugaji nyuki, mapato ya Serikali kutokana na vibali vya mbao.