Mjasiriamali ambaye amepata mafunzo kutoka kwa MKURABITA Furaha Juma Abdalla akiwauzia bidhaa anazozalisha baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA waliomtembelea kwake Chukwani Zanzibar kujua maendeleo ya shughuli zake.……………………..Na Faki Mjaka-Maelezo ZanzibarSerikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Wizara ya Biashara na Viwanda, Tume ya Mipango Zanzibar na Ofisi ya Mpango wa kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Taanzania (MKURABITA) zitaendeleza azma yake muhimu ya kuhamasisha urasimishaji wa Wafanyabiashara wadogo wadogo wa Zanzibar ili kuzifanya biashara zao kutambulika kisheria.Kwa kufanya hivyo kutawawezesha Wajasiriamali mbali mbali kufanya biashara endelevu zinazowakomboa kiuchumi na kuepuka kufanya biashara ya kimazoea zisizoleta tija.Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Viwanda Juma Reli ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA iliyomtembelea Ofisini kwake Migombani ikiwa ni mwendelezo wa kukagua shughuli zinazofanywa na Kamati hiyo visiwani Zanzibar.Amesema kwa Zanzibar kazi za urasimishaji hufanyika kwa kushirikiana na Ofisi za Wilaya na Halmashauri husika ambapo Wafanyabiashara hupatiwa mafunzo maalum ya urasimishaji.“Unapokuwa rasmi unaweza kupata mkopo kirahisi, ukipata mkopo pia kuna uwezekanao wa biashara kukua na pato la Taifa pia huongezeka” alifafanua Katibu Juma Reli.Kwa upande wake Mkurugenzi wa Biashara na ukuzaji masoko Khamis Ahmad Shauri amesema jumla ya Wafanyabiashara wadogo 154 walipatiwa mafunzo ya urasimishaji Unguja na Pemba kwa mwaka 2018/2019Amefahamisha kuwa Wafanyabiashara wanaporasimishwa hupata fursa ya kuweza kukopa Mitaji katika vyanzo mbalimbali ikiwemo Benki ambayo huwasaidia kuziendeleza biashara zao kwa faida yao na vizazi vyao.Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya uongozi ya MKURABITA Balozi Daniel Ole Njolay ameishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupunguza gharama za uanzishwaji wa biashara kwa wananchi ikiwemo ukataji wa Leseni ili kuyafanya mazingira ya biashara kuwa rahisi.Mratibu wa MKURABITA Tanzania Dkt. Seraphia Mgembe ameiomba Wizara ya Viwanda na Biashara Zanzibar kuandaa mijadala ya wazi kwa wananachi walionufaika na MKURABITA Zanzibar ili iwahamasishe wananchi wengine kurasimisha biashara na rasilimali zao.Awali Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya MKURABITA walimtembelea Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar Mwita M. Mwita na kufanya mazungumzo naye ambapo aliwaeleza kuwa Ofisi yake tayari imeratibu na kufanya utambuzi wa Viwanja zaidi ya 10,000.Amesema baada ya utambuzi huo Serikali ya Mapinduzi ipo mbioni kutoa hati za Viwanja hivyo kwa wananchi ili kufanya shughuli zao na kuepuka migogoro ya ardhi.Kamati hiyo pia ilipata fursa ya kutembelea Wajasiriamali walionufaika na MKURABITA na kuona maendeleo yao ambapo pia walielezea changamoto ya masoko kwa bidhaa wanazozizalisha.Mpango wa kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Taanzania (MKURABITA) ulianzishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2004 ikiwa ni mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini Tanzania MKUKUTA na MKUZA ambapo walengwa hutumia raslimali na biashara zao zilizorasmishwa katika kujipatia mitaji, soko na fursa zingine.