Dkt.
Migiro apokea vifaa vya mafunzo ya utabibu vyenye thamani ya Tsh. milioni 130 Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza ulipokea kifaa
muhimu cha kufundishia madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa sekta ya afya,
pamoja na vitabu vya kitabibu kutoka katika Jumuiya ya Watanzania waishio
Uingereza wanaofanya kazi katika sekta ya afya (Tanzania United Kingdom Health
Diaspora Association – TUHEDA). Kifaa hicho ni sanamu ya binadamu ambayo
inaendeshwa na programu maalumu za kompyuta zinazowezesha wataalamu mbalimbali
wa afya kupata uhalisia wa hali ya magonjwa kama ambavyo wangeupata kutoka kwa
mgonjwa aliye hai. Sanamu hiyo iliyopewa jina la ‘Msafiri’ na Ubalozi, ina
uwezo wa kupumua, kutoa sauti ya mapafu kama mtu mwenye pumu, homa ya mapafu,
au mapigo ya moyo yanayoweza kuashiria shinikizo la juu au la chini la damu,
sawa na mgonjwa halisi. Upatikanaji wa sanamu hiyo umefanikishwa na mwanachama
wa TUHEDA, Dkt. Nasibu Mwande, mtaalamu wa masuala ya ajali na magonjwa ya
dharura (Accidents and Emergency), anayefanya kazi ya udaktari hapa Uingereza. ‘Msafiri’ ana thamani ya pauni za Uingereza zisizopungua 30,000 (sawa na
shilingi za Tanzania zipatazo milioni mia moja), ana umbo la kawaida la
binadamu na uzito wa kilo 60. Ubalozi umetaarifiwa kuwa sanamu hiyo ni ya
kwanza nchini Tanzania katika ufundishaji wa kitabibu. Kupatikana kwa ‘Msafiri’ kutasaidia sana kupunguza
makosa ya kibinadamu yanayoweza kufanywa na madaktari, wauguzi na wataalamu
wengine kwani ‘Msafiri’ anaweza kutumika kutoa mafunzo ya kitabibu kwa mfano
halisi wa magonjwa mbalimbali bila ya madhara ambayo yangetokea kama wataalamu
wa utabibu wangetegemea kujifunza kupitia mgonjwa aliye hai. TUHEDA pia
wamekabidhi vitabu muhimu mia tatu vinavyotumika kama rejea kwa madaktari
wakati wa kuamua mgonjwa apewe dawa gani, dawa zipi zinaweza kutumika kwa
pamoja bila madhara, na zitolewe kwa kiwango gani. Vitabu hivyo vina thamani
inayokaribia pauni 9,000 sawa na shilingi za Tanzania zipatazo milioni 30. Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, |