Home Michezo TAIFA STARS YAANZA VIBAYA AFCON,YACHAPWA 2-0 NA SENEGAL

TAIFA STARS YAANZA VIBAYA AFCON,YACHAPWA 2-0 NA SENEGAL

0

Na Mwandishi Wetu, CAIRO
TANZANIA imeanza vibaya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Senegal katika mchezo wa Kundi A usiku huu Uwanja wa Juni 30 mjini Cairo, Misri.
Huo unakuwa mchezo wa kwanza wa Taifa Stars kumaliza bila kupata bao kwenye fainali za AFCON baada ya mwaka 1980 mjini Lagos kufunga bao moja katika kila mchezo ikifungwa 3-1 na wenyeji, Nigeria, 2-1 na Misri na kutoa sare ya 1-1 na Ivory Coast katika mechi zake za Kundi A.
Senegal ilipata pigo dakika ya 23 baada ya beki wake, Salif Sane wa Schalke 04 ya Ujerumani kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Cheikhou Kouyate wa Crystal Palace ya England.

Sane aliangukia goti wakati anagombea mpira wa juu dhidi ya mshambuliaji wa Tanzania, John Raphael Bocco anayechezea klabu ya Simba ya nyumbani na kuumia kabla ya kutolewa na machela.
Pamoja na hayo, mshambuliaji wa Monaco ya Ufaransa, Keita Balde anayecheza kwa mkopo Inter Milan ya Italia alianza kuifungia Senegal bao la kwanza dakika ya 28 akimalizia kazi nzuri ya kiungo wa Everton ya England, Idrissa Gana Gueye.
Kipindi cha pili timu zote zilirudi kama zilivyomaliza dakika 45 za kwanza na mambo yakazidi kuwa mabaya kwa Taifa Stars baada ya kiungo wa Club Brugge ya Ubelgiji, Krepin Diatta kuwafungia bao la pili Simba wa Teranga dakika ya 64 kwa shuti la mbali lililowapita walinzi wa Stars na kipa wao, Aishi Manula mashuhuda.
Taifa Stars wakiongozwa na Nahodha wake, Mbwana Ally Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji walijitahidi kutafuta japo bao la kufutia machozi, lakini hawakufanikiwa mbele ya ukuta imara wa Senegal inayoshika nafasi ya 22 kwa ubora FIFA.
Taifa Stars inayoshika nafasi ya 131 FIFA, ambayo inafundishwa na nyota wa zamani wa Nigeria na Barcelona, winga Emmanuel Amunike ilizidiwa kimchezo na Simba wa Teranga walio chini ya mchezaji wao wa zamani na klabu za Birmingham City na Portsmouth za England, aliyekuwa kiungo wa ulinzi, Aliou Cisse.
Taifa Stars haikulenga shuti hata moja langoni mwa Senegal, ilipiga mashuti matatu tu nje, ilipata kona tatu, ilicheza faulo 22 na ilioteamara moja.
Simba wa Teranga pamoja na kufunga mabao mawili, walilenga mashuti saba langoni mwa Stars, walipiga nje mara 11, walipata kona sita na waliotea mara mbili, ingawa nao walicheza faulo 17.
Mchezo mwingine wa Kundi A unafuatia Saa 5:00 usiku kati ya Algeria na Kenya Uwanja wa Juni 30, baada ya mapema leo, Morocco kuichapa 1-0 Namibia katika mchezo wa Kundi D, bao la kujifunga la Itamunua Keimuine Uwanja wa Al Salam mjini Cairo.
Taifa Stars watateremka tena dimbani Juni 27 kumenyana na jirani zao, Kenya Saa 5:00 usiku kabla ya kumalizia na Algeria Julai 1.
Kikosi cha Senegal kilikuwa; Edouard Mendy, Kalidou Koulibaly, Salif Sane/ Cheikhou Kouyate dk23, Youssouf Sabaly, Moussa Wague, Idrissa Gueye, Badou N’Diaye, M’Baye Niang/ Moussa Konate dk83, Keita Balde/Sada Thioub dk73, Ismaila Sarr na Krepin Diatta.
Tanzania; Aishi Manula, Hassan Kessy, Gardiel Michael, David Mwantika, Kelvin Yondani, Mudathir Yahya/Frank Domayo dk84, Himid Mao, Feisal Salum/Farid Mussa dk44, John Bocco, Mbwana Samatta na Simon Msuva/Thomas Ulimwengu dk66.