Home Michezo WATUMISHI NI MUHIMU KUSHIRIKI MICHEZO-MAJALIWA

WATUMISHI NI MUHIMU KUSHIRIKI MICHEZO-MAJALIWA

0

Martin Massawe wa NMB akimlamba chenga Abdallah Aman wa Bunge (kushoto) katika mechi ya soka ya Bonanza la Benki ya NMB na Wabunge kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma Juni 22, 2019. Bunge ilishinda 5-3.

Abdallah Aman wa Bunge (kushoto) akizuia mpira huku akizongwa na Martin Massawe wa Bunge katika mechi ya soka ya Bonanza la Benki ya NMB na Wabunge iliyochezwa kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma Juni 22, 2019. Bunge ilishinda 5-3.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Kikombe nahodha wa timu ya soka ya Bunge, Cosato Chumi baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa 5-3 dhidi ya timu ya NMB katika mchi ya Bonanza la Benki ya NMB na Wabunge kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Juni 22, 2019. Kushoto ni Naibu Spika Dkt. Tulia Ackson Mwansasu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (kushoto) wakimtazama nahodha wa timu ya Soka ya Bunge, Cosato Chumi aliponyanyua kikombe cha ushindi wa mechi ya soka ya Bonanza la Benki ya NMB na Wabunge kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Juni 22, 2019. Bunge ilishinda 5 – 3. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 …………………..

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema ni muhimu kwa watumishi kushiriki katika michezo mbalimbali kwa kuwa inaimarisha afya pamoja na kudumisha mshikamano.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Juni 22, 2019) wakati wa bonanza kati ya Wabunge na watumishi wa benki ya NMB lililofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema mbali na kuimarisha afya kwa watumishi na wabunge, pia michezo inasaidia katika kuimarisha mshikamano baina ya benki hiyo pamoja na wateja.

Akizungumzia kuhusu utendaji wa benki ya NMB, amesema imekuwa ikishirikiana na Serikali kuwaelimisha wakulima umuhimu wa kufungua akaunti na kujiwekea akiba.

“Benki ya NMB ni benki pekee iliyomudu kufungua matawi hadi maeneo ya vijijini, hivyo kurahisha upatikanaji wa huduma kwa watumishi na wananchi waishio maeneo hayo.”

Michezo iliyochezwa katika bonanza hilo ni mpira wa miguu ambapo timu ya Bunge ilishinda baada ya kuifunga timu ya benki ya NMB magoli matano kwa matatu.

Kwa upande wa mchezo wa mpira wa pete timu ya Bunge iliibuka na ushindi baada ya kuifunga timu ya NMB magoli 25 kwa 18, huku katika mchezo wa mpira wa kikapu timu ya NMB ilishinda baada ya kuifunga Bunge vikapu 52 kwa 51.

Katika mchezo wa kuvuta kamba timu ya Wabunge Wanawake na Wanaume waliibuka na ushindi baada ya kuzishinda timu za NMB.