Home Mchanganyiko WAKALA WA VIPIMO YASISITIZA MATUMIZI YA VIPIMO SAHIHI KATIKA UNUNUZI WA ZAO...

WAKALA WA VIPIMO YASISITIZA MATUMIZI YA VIPIMO SAHIHI KATIKA UNUNUZI WA ZAO LA PAMBA TABORA

0

Meneja wa Wakala wa Vipimo Tabora akitoa elimu ya matumizi sahihi ya mizani kwa Wakulima wa kijiji cha Mtunguru waliokuja kuuza pamba zao katika Chama cha msingi cha ushirika cha Nguzujise

Afisa Vipimo Mkoa wa Tabora akihakiki usahihi wa mizani inayotumika kununulia pamba kwa kutumia jiwe maalumu la Wakala wa Vipimo.

Afisa Vipimo Mkoa wa Tabora akihakiki usahihi wa mizani inayotumika kununulia pamba kwa kutumia jiwe maalumu la Wakala wa Vipimo

Wananchi wakioneshwa alama za kukagua ili kubaini usahihi wa mizani kabla ya kuuza pamba

Stika ya Wakala wa Vipimo ikiwa imebandikwa katika mizani iliyohakikiwa

Pamba ikiwa tayari kwa ajili ya upimaji

……………………..

Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Tabora inaendelea kufanya uhakiki wa mizani ya vyama vya msingi vya ushirika pamoja na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo katika Wilaya mbalimbali za mkoa wa Tabora ili kuweza kuwalinda wakulima wa zao la pamba waweze kupata faida kwa kuuza mazao yao (pamba) kwakutumia vipimo mizani sahihi iliyohakikiwa na wakala wa Vipimo.

Meneja wa WMA Tabora ndugu Mrisho Mandari, amesema kuwa mpaka sasa Wakala wa Vipimo Tabora imeshafanya uhakiki wa mizani ya vyama vya msingi vya ushirika katika Wilaya tano za Mkoa wa Tabora ambazo ni Igunga, Nzega, Uyui, Urambo pamoja na Kaliua. Katika wilaya zote Jumla ya Mizani 158 imehakikiwa na Wakala wa Vipimo na kusambazwa katika vituo vyote vya kununulia pamba Mkoani hapo.

Amesema kuwa, Kati ya Mizani 158 iliyohakikiwa jumla ya mizani 130 ilipitishwa haikubainika kuwa na tatizo lolote, na mizani 18 ilikutwa na hitilafu ndogo ndogo ambapo baadaye zilirekebishwa na 16 kati ya hizo zilifikia wigo wa usahihi. Mizani miwili ilikataliwa kabisa kutumika kutokana na matatizo yake kuwa makubwa.

Ndugu Mrisho Mandari, amesema kuwa mara baada ya kukamilisha uhakiki wa mizani ya vyama vya msingi vya ushirika (AMCOS), sasa wanatoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo kwa Wakulima wa pamba na wanachi wote kwa ujumla ili waweze kutambua mambo muhimu ya kuzingatia mara wanapoenda kuuza pamba katika vituo maalumu vilivyoandaliwa.

Pia, amewaasa wakulima wawe makini pindi wanapoenda kuuza pamba kwa kuhakikisha mizani inasoma sufuri (0) kabla ya kuanza upimaji kwa kutumia mizani ya digitali. Mara baada ya kupima furushi la pamba mizani inatakiwa kurudi katika sufuri, na wahakikishe mizani haisomi hasi (-) baada ya kutoa mzigo na ikitokea imesoma hasi mwambie karani  anayesimamia mizani aweze kuizima na kuiwasha tena mizani hiyo kisha zoezi la upimaji liendelee.

Wakala wa vipimo inaendelea kuboresha ulinzi katika mizani zinazotumika katika ununuzi wa zao la pamba, kwa mizani iliyohakikiwa na kukudhi vigezo inawekewa stika maalumu ya Wakala wa Vipimo pamoja na kufunga lakiri katika maeneo muhimu ya mizani ili kuzuia mizani isije ikachakachuliwa na wanunuzi wa pamba wasio waaminifu.

Vilevile, amewataka wanunuzi wa pamba waweze kujiepusha na viendo vya dhuruma kwa wakulima wa pamba kwa kutumia mizani ambazo hazija hakikiwa na kupata idhini ya kutumika katika msimu wa ununuzi wa pamba. Amewakumbusha kuwa kwa sasa sheria ya vipimo sura na. 340 na mapitio yake ya mwaka 2002 imefanyiwa marekebisho na adhabu zimekuwa kali ambapo ukikutwa na kosa la kuchezea mizani na ukakiri faini yake ni kiasi kisichozidi shilingi milioni ishirini (20,000,000/=) kwa kosa la kwanza na kiasi kisichozidi milioni hamsini (50,000,000/=) kwa mkosaji wa kosa la kujirudia.

Zoezi hili la uhakiki wa mizani na utoaji elimu kwa wakulima wa pamba ni zoezi endelevu ambalo hufanyika mara kwa mara ili kuwalinda wakulima wa pamba na hufanyika kabla ya kuanza kwa msimu wa ununuzi wa pamba na mara baada ya kuanza kwa msimu maafisa vipimo hupita katika vituo mbalimbali vinavyotumika kununulia pamba na kujiridhisha kama mizani inatumika kwa usahihi bila kupunja kama ilivyo hakikiwa.

Wakala wa vipimo inatoa wito kwa Wafanyabiashara na Wakulima wote kuhakikisha wanazingatia matumizi ya vipimo sahihi na kujiepusha na uchezeaji wa vipimo na endapo mkulima utakutana na udanganyifu wa aina yeyote atoe taarifa katika ofisi zetu za wakala wa vipimo zilizopo makao makuu ya mikoa yote Tanzania Bara au kupitia namba yetu ya bure kabisa ambayo ni 0800 11 00 97.