Home Mchanganyiko SERIKALI HAITOSITA KUMCHUKULIA HATUA MTU YEYOTE ATAKAYEJIHUSISHA NA MASUALA YA RUSHWA

SERIKALI HAITOSITA KUMCHUKULIA HATUA MTU YEYOTE ATAKAYEJIHUSISHA NA MASUALA YA RUSHWA

0

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb), akifungua
mjadala kuhusu Kuelekea Msimamo wa Pamoja wa Afrika kuhusu
Urejeshwaji Mali wakati wa Kongamano la Siku Maalum ya
Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika iliyoadhimishwa kitaifa
jijini Dodoma.

Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Siku Maalum ya Mapambano
Dhidi ya Rushwa Barani Afrika, wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt
(Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb), alipokuwa akifungua mjadala
kuhusu Kuelekea Msimamo wa Pamoja wa Afrika kuhusu Urejeshwaji
Mali wakati wa kongamano hilo jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Diwani
Athumani akitoa maelezo ya awali kuhusu Siku Maalumu ya
Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika wakati wa Kongamano la
siku hiyo iliyoadhimishwa kitaifa jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb) akimkabidhi
mwongozo wa utendaji kazi mmoja wa wajumbe wa kamati ya
uadilifu ya Chuo Kikuu cha Dodoma wakati wa Kongamano la Siku
Maalum ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika
iliyoadhimishwa kitaifa jijini Dodoma.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Kapt (Mst) Mhe. George Mkuchika (Mb) akipokea hati
ya utambuzi wa mchango wake katika mapambano dhidi ya rushwa
toka kwa viongozi wa Klabu ya Wapinga Rushwa ya Chuo Kikuu cha
Dodoma, wakati wa Kongamano la Siku Maalum ya Mapambano
Dhidi ya Rushwa Barani Afrika iliyoadhimishwa kitaifa jijini Dodoma.

************

Serikali haitosita kumchulia hatua za kisheria mtu yeyote bila kujali wadhifa
alionao pindi atakapobainika kujihusisha na masuala ya rushwa ambayo ni
kikwazo kwa maendeleo ya taifa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Kapt (Mst) George Mkuchika
(Mb) alipokuwa akifungua mjadala kuhusu “Kuelekea Msimamo wa Pamoja
wa Afrika kuhusu Urejeshwaji Mali” wakati wa Kongamano la Siku Maalum
ya Mapambano Dhidi ya Rushwa Barani Afrika iliyoadhimishwa kitaifa jijini
Dodoma.

Mhe. Mkuchika amesema, baadhi ya watu wanadhani kuwa, Serikali
inashughulika na wala rushwa wadogo wadogo tu, ukweli ni kwamba, wapo
baadhi ya walioshika nyadhifa za uwaziri wamelazimika kuwajibika na
kutumikia kifungo kutokana na suala la rushwa na ubadhirifu wa mali za
umma.

Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, hatua dhidi ya waliobainika na masuala
ya rushwa ni matokeo ya uanzishwaji wa Mahakama ya wala rushwa na
wahujumu uchumi iliyoanzishwa, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi
ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

“Tumeanza kupiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa na matokeo
yameonekana, hivyo tusibweteke kwasababu bado tuhahitaji kuendeleza
mapambano hayo,” Mhe. Mkuchika amesisitiza.

 

Mhe. Mkuchika ameipongeza Klabu ya Wapinga Rushwa ya Chuo Kikuu
cha Dodoma kwa kuwa hai na yenye nguvu katika mapambano dhidi ya
rushwa, na kutoa wito kwa klabu nyingine katika taasisi za elimu ya juu
kuiga mfano huo.

Aidha, Mhe. Mkuchika amewahimiza wanataaluma nchini, klabu za
wapinga rushwa katika vyuo vya elimu ya juu, TAKUKURU pamoja na
wadau wengine kuendelea kufanya tafiti kuhusu rushwa na masuala ya
utawala bora ili kutoa mapendekezo ya namna Serikali na wananchi
watakavyoshiriki katika mapambano dhidi ya rushwa.

Mada kuhusu historia ya vita dhidi ya rushwa Tanzania na urejeshaji wa
mali zilizopatikana kwa njia ya rushwa barani Afrika ziliwasilishwa katika
kongamano hilo.