Home Michezo Ruvuma, Songwe Zatinga Fainali UMISSETA 2019

Ruvuma, Songwe Zatinga Fainali UMISSETA 2019

0

Mabingwa UMISSETA mwaka 2017 timu ya soka wavulana ya mkoa wa Songwe wakifuraia ushindi baada ya kuifunga kwa penati timu ya mkoa wa Mwanza

Golikipa wa Songwe Joseph shibanda akipangua shuti kali la penati lililopigwa na Felician Lucas wa Mwanza na kuipa ushindi timu yake ya Songwe kwa jumla ya magoli 4-3

Patashika katika mchezo wa mpira wa kikapu wasichana baina ya timu ya mkoa wa dar es salaam dhidi ya timu ya mkoa wa Morogoro ambapo Dar es salaam waliilaza Morogoro kwa 38-17

…………………

Na Mathew Kwembe, Mtwara

Timu za mpira wa miguu za wavulana kutoka mikoa ya Ruvuma na Songwe ndizo zitakazocheza hatua ya fainali kumtafuta bingwa wa UMISSETA mwaka huu, mchezo unaotarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Nangwanda  ijumaa tarehe 21 juni 2019.

Ruvuma ndiyo walikuwa wa kwanza kufuzu hatua hiyo baada ya kuifunga Lindi kwa magoli 2-0. Magoli ya Ruvuma yakifungwa na Said Bakari dakika ya 29 na John Ching’uku alifunga goli la pili dakika ya 59.

Katika mchezo baina ya Mwanza na songwe ulilazimika kuamuliwa kwa mikwaju ya penati baada timu hizo kutoka suluhu ya bila kufungana katika dakika 90 za mchezo na hatimaye Songwe kushinda kwa penati 4-3.

Shujaa  wa mchezo huo alikuwa ni golikipa wa Songwe Joseph Shibanda ambaye ndiye aliyewanyamazisha mashabiki wa Mwanza baada ya kudaka shuti kali la Felician Lucas wa Mwanza.

Penati nyingine kwa upande wa Songwe zilifungwa na Pascal Adriano, Joseph Shibanda, Michael kabuki pamoja na Justine Mwambungu huku penati ya Sekelo Kalinga ‘’kichuya mtoto’’ ikipanguliwa na golikipa wa mwanza.

Waliofanikiwa kufunga magoli kwa upande wa timu ya Mwanza ni  Nassoro Omary, Frank Faustino na Boniface Ernest huku waliokosa kwa upande wa Mwanza ni Mashinyali Maira, na Felician Lucas.

Kocha wa Songwe, Mwalimu PrayGod Lugenge amesema kuwa amefurahia timu yake kuingia fainali  kwani walijiandaa kwa muda mrefu baada ya kufanya mazoezi kwa muda mrefu.

Alisema kuwa hashangazwi na timu yake kufika hatua hiyo kwani mwaka 2017 wakati wanashiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza walifanikiwa kushinda mechi zao na hatimaye walitwaa kombe hilo ikiwa ni mara yao ya kwanza kushiriki mashindano hayo.

Lugenge alisema kuwa timu yake pamoja na kucheza vizuri kwenye mchezo huo  ndani ya dakika 90 walilazimika kusubiri mchezo huo uamuliwe kwa penati baada ya timu yake kufanya mashambuzi mengi dhidi ya Mwanza.

Mwalimu huyo kutoka shule ya sekondari J.K Nyerere iliyopo Tunduma aliwataka wadau wa soka nchini hususan TFF kutafuta vipaji katika maeneo mengi nchini badala ya kung’ang’ania wachezaji wa Dar es salaam peke yake.

Amesema timu ya Songwe ina fursa ya kufanya vizuri kwani wachezaji wake wengi wanaundwa na timu nne za mkoa huo na hivyo wachezaji wake wengi wanafahamiana kwani wamecheza muda mrefu.

Aidha Kocha huyo wa Songwe ameisifu kamati ya kuratibu mashindano ya UMISSETA na  TAMISEMI kwa namna ilivyokuwa makini kuhakikisha kuwa mashindano ya mwaka huu hayatawaliwi na  mamluki.

Amesema mfumo wa kielektroniki uliotumiwa mwaka huu umerejesha msisimko uliokuwepo miaka ya nyuma ambapo wachezaji wanaoshiriki mashindano hayo ni wale wanaosoma katika shule za sekondari nchini.

Kwa upande wake nahodha wa Songwe Joseph Shibanda naye ameipongeza serikali kwa usimamizi thabiti wa michezo hiyo ambapo amesema kuwa kutokana na namna usimamizi ulivyokuwa mzuri utawezesha kupatikana kwa bingwa wa kweli na pia kuwezesha mikoa mingine kama Simiyu, Geita na Njombe kuwa na nafasi ya kushinda kombe hilo.

Wakati huo huo matokeo ya mpira wa kikapu yanaonyesha kuwa timu za kutoka mikoa ya Pwani na Shinyanga zitacheza hatua ya fainali kwa upande wa wavulana na timu za Mwanza na Dar es salaam zitakutana katika hatua hiyo kwa upande  wa wasichana.

Katika matokeo ya nusu fainali kwa kikapu wavulana Pwani iliwafunga Unguja kwa 66-32 na Tanga ilifungwa na Shinyanga kwa 47-55.

Kwa upande wa kikapu wasichana Mwanza iliwafunga Kilimanjaro 38-18 na Dar es salaam iliwafunga Morogoro kwa 38-17.