Home Mchanganyiko TANZANIA YAUNGANA NA MATAIFA MENGINE BARANI AFRIKA WANACHAMA WA UMOJA WA AFRIKA...

TANZANIA YAUNGANA NA MATAIFA MENGINE BARANI AFRIKA WANACHAMA WA UMOJA WA AFRIKA KUADHIMISHA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA KUANZIA LEO JUNI 16 HADI 23-2019

0

Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.

Tanzania inaungana na Mataifa mengine wanachama wa Umoja wa Afrika katika  kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma barani Afrika ambayo yameanza leo Jumapili Mwezi Juni 16  ambapo kilele chake itakuwa Juni 23,jijini Nairobi nchini Kenya kwa Bara zima la Afrika.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma,Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi  wa Umma Kapt.George Mkuchika alisema katika wiki ya utumishi wa Umma mwaka 2019,Ofisi yake imewalekeza watendaji wa taasisi za Umma kuadhimisha wiki ya utumishi wa Umma katika maeneo yao ya kazi  ili kusikiliza maoni na changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na kukutana na wadau wa nje kwa lengo la kupata mrejesho wa huduma wanazozitoa.

Aidha,Waziri Kapt.Mkuchika alisema ili kujenga mahusiano mazuri na jamii ,Taasisi za umma zinaweza kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma kwa kufanya shughuli za kijamii kama vile usafi wa Mazingira katika maeneo mbalimbali hususan hospitalini,sokoni na katika fukwe za mito na bahari zilizo jirani na maeneo yao ya kazi.

Waziri Kapt.Mkuchika ameyataja baadhi ya Malengo ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Barani Afrika ni kutafakari juu ya wajibu ,dhima,dira,malengo ya utumishi wa umma ,mikakati,mchango na umuhimu wa watumishi wa umma,changamoto zao na kuhamasisha kuendelea kufanya kazi nzuri  katika ujenzi wa Taifa pamoja na kupata mirejesho kutoka kwa wananchi na wadau wanaohudumiwa na taasisi za umma ili kurekebisha kasoro za utendaji zinazosababisha malalamiko ya wateja.

Waziri Kapt.Mkuchika mara baada ya kilele cha Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma ameziagiza Sekretarieti za mikoa ,Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi zote za Umma kuwasilisha taarifa ya namna walivyoshiriki kwa makatibu wakuu wa Wizara zao  ambao wataunganisha taarifa zote na kuziwasilisha kwa katibu mkuu ofisi ya Rais ,Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili Serikali iweze kutumia taarifa hizo kuboresha utendaji kazi.

Kwa Mwaka 2019 Tanzania ni Kinara maadhimsho ya Wiki ya Utumishi wa Umma barani Afrika yatakayofanyika Nairobi Kenya kuanzia tarehe 21 hadi 23,2019  na shughuli zitakazofanyika ni pamoja na maonyesho ya shughuli za ubunifu huku taasisi zitakazoshiriki katika maadhimisho hayo ni zile huduma zake zinazolenga moja kwa moja kauli mbiu ya mwaka huu.

Chimbuko la  maadhimisho ya  wiki ya utumishi wa Umma   ambayo huadhimishwa kila baada ya miaka miwili barani Afrika ni uamuzi wa mkutano wa Mawaziri  wenye dhamana ya utumishi ,uliofanyika Tangiers nchini Morocco mwaka 1994 ambapo ulizitaka nchi za Afrika kusherehekea kwa kauli mbiu moja katika bara zima la Afrika ambapo kwa kauli mbiu mwaka 2019 ni “Uhusiano kati ya Uwezeshaji wa vijana na usimamizi wa Masuala ya Uhamiaji,Kujenga Utamaduni wa Utawala Bora ,Matumizi ya TEHAMA  na Ubunifu katika utoaji Huduma Jumuishi.”