Home Mchanganyiko OLE MILLYA AFAGILIA MIRADI YA KIMKAKATI YA MAGUFULI

OLE MILLYA AFAGILIA MIRADI YA KIMKAKATI YA MAGUFULI

0

Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya (kushoto) akimsikiliza Ofisa mtendaji wa kata ya Orkesumet, Edmond Tibiita (kulia) akielezea miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanyika eneo hilo, katikati ni Diwani wa kata hiyo Sendeu Laizer.

Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya akifurahi baada ya wananchi wa Kata ya Edonyoengijape kumkabidhi zawadi ya kondoo kama shukurani kwa kutetea maslahi ya jamii ya wafugaji akiwa bungeni.

Wananchi wa mji mdogo wa Orkesumet wakimpokea mbunge wa jimbo la Simanjiro mkoani Manyara, James Ole Millya ambaye kwa muda wa zaidi ya wiki moja alikuwa kwenye ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, kuzungumza na jamii na kusikiliza kero, malalamiko na changamoto zao.
************************************
Mbunge wa jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, James Ole Millya amesema miradi mikubwa mitano ya kimkakati inayotekelezwa na iliyoahidiwa na Serikali ya Rais John Magufuli Wilayani Simanjiro ndiyo imesababisha yeye aondoke Chadema na kuhamia CCM.
Ole Millya akizungumza na wananchi wa mji mdogo wa Orkesumet alisema aliamua kuhama kama shukrani na kumuunga mkono Rais Magufuli kutokana na maendeleo hayo. 
Alitaja miradi hiyo ya maendeleo ni baada ya kusoma ilani ya CCM chini ya serikali ya Rais John Magufuli juu ya ujenzi wa barabara ya lami ya Arusha, Komolo, Terrat na Mirerani, Orkesumet, Kiteto hadi Kongwa mkoani Dodoma. 
Alisema mradi mkubwa wa maji wa mto Pangani (Ruvu) hadi Orkesumet wenye thamani ya sh41 bilioni unaoendelea, ukuta wa madini ya Tanzanite ambapo badala ya kukusanya sh70 milioni kwa mwaka sasa inakusanywa sh2.1 bilioni na wananchi wanafaidika nayo. 
“Mradi mwingine ni katika hospitali mpya 60 nchi nzima zinazojengwa na sisi Simanjiro tumepata hospitali ya wilaya tukitengewa sh1.5 bilioni, na ujenzi unaendelea kwa kasi kwenye kata ya Langai kwani hatukuwa na hospitali tangu wilaya igawanywe kutoka Kiteto,” alisema Ole Millya. 
Alitaja sababu nyingine ni mgogoro baina ya wafugaji wa kata ya Loiborsiret na hifadhi ya Taifa ya Tarangire na pori la akiba la Mkungunero ulisababisha waishi kwa hofu na manyanyaso ila Rais Magufuli akaingilia kati na kuwasaidia wafugaji nchini. 
“Kilio cha wafugaji kupatiwa ufumbuzi baada ya Rais John Pombe Magufuli kuunda Tume ya Mawaziri nane wakiongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kufuatilia kero za wafugaji wa Kimotorok,” alisema Ole Millya. 
Alisema kutokana na maemdeleo hayo yanayofanyika Simanjiro aliamua kuhama Chadema na kurudi CCM chama ambacho alikuwepo na kuwahi kuwa Mwenyekiti wa jumuiya ya UVCCM mkoani Arusha.
“Baada ya kuona ubabaishaji na ubaguzi unafanyika CCM wilayani Simanjiro niliamua kuhamia Chadema na ninawashukuru mkanichagua mimi mtoto wa masikini ambaye sikuwapa hata shilingi moja,” alisema Ole Millya.
Diwani wa kata ya Orkesumet, Sendeu Laizer alimshukuru Ole Millya kwa kuwasemea bungeni hadi wakapata sh200 milioni za kituo cha afya na Waziri wa Tamisemi Selemani Jafo ameahidi kuwapatia kilomita mbili za barabara ya lami.
Laizer alisema pia sekondari ya Simanjiro imeboreshwa na mwaka huu itapokea wanafunzi wapya wa kidato cha tano kwani mabweni na bwalo la kulia chakula yameshakamilika.
Alisema mwaka 2015 baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Mapinduzi walikuwa wanasoma chini ya miti lakini serikali ya Rais John Magufuli ikawajengea madarasa saba na kumaliza changamoto hiyo.