Mwanariadha Regina Deogratius kutoka mkoa wa Pwani akimaliza mbio za mita 1500 na kujinyakulia medali ya dhahabu katika viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara leo asubuhi
Mwanariadha Teresia Nicholaus wa Singida ambaye alishika nafasi ya pili katika mbio za mita 1500 akivuka mstari kuashiria kukamilika kwa mbio hizo. Teresia alionekana kuwa kivutio kwenye mbio hizo kutokana na kasi aliyoionyesha kulinganisha na umbo lake.
Mshindi wa kwanza hadi wa tatu kwa upande wa wavulana, wakimaliza mbio za mita 1500 leo asubuhi katika viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara.
*******************
Na Mathew Kwembe, Mtwara
Mkoa wa Dar es salaam umeendelea kutamba katika mashindano ya UMISSETA yanayoendelea katika viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara kufuatia mkoa huo kutoa mshindi wa kwanza na wa pili katika fainali za mbio za mita 100 kwa upande wa wavulana katika fainali zilifanyika leo asubuhi.
Mwanariadha Ismail Tosil akitumia sekunde 11:49 alifanikiwa kushika nafasi ya kwanza katika mbio hizo na hivyo kujitwalia medali ya dhahabu, huku mwanariadha mwenzake Elias Silverster ambaye alitumia sekunde 11: 50 pia kutoka Dar es salaam kushika nafasi ya pili na kujinyakulia medali ya fedha, huku nafasi ya tatu ilichukuliwa na mwanariadha Geofrey Maganga kutoka mkoani Dodoma aliyetumia sekunde 11:68 na kujinyakulia medali ya shaba.
Kwa upande wa wasichana, Mwanariadha Emmy Hosseah kutoka mkoani Singida amefanikiwa kutwaa medali ya dhahabu katika mbio za mita 100 baada ya kuwaacha nyuma wenzake, Leocadia Joho kutoka Tabora aliyeshika nafasi ya pili na Zawadi Juma wa Mara aliyeshika nafasi ya tatu.
Emmy alifanikiwa kumaliza mbio hizo baada ya kutumia sekunde 13:16, huku Leokadia Joho akitumia sekunde 13:48 na Zawadi Juma aliyejitwalia medali ya shaba alitumia sekunde 13:70.
Katika mbio za mita 1500, mwanariadha Japhet John kutoka mkoani Singida alitwaa medali ya dhahabu kwa kushika nafasi ya kwanza baada ya kutumia dakika 4:12:31, huku nafasi ya pili kwa upande wa wavulana ikishikwa na Lusengulano Faida kutoka Mwanza aliyetumia dakika 4:12:88, na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Emanuel Petro kutoka Shinyanga ambaye alitumia dakika 4:13:58.
Katika mbio za mita 1500 wasichana, aliyetwaa medali ya dhahabu ni mwanariadha Regina Deogratius kutoka Pwani ambaye alimaliza mbio hizo baada ya kutumia dakika 4:44:67, nafasi ya pili ikichukuliwa na Teresia Nicholaus kutoka Singida ambaye alitumia dakika 4:49:25 na nafasi ya tatu ilikwenda kwa mwanariadha Yusta Ninga kutoka mkoa wa Manyara baada ya kutumia dakika 4:50:49.