Home Michezo fainali za mita 200 na 800 umisseta

fainali za mita 200 na 800 umisseta

0

Ismail Hussein Tosiri wa Dar es salaam akimaliza mbio za mita 200 mbele ya wenzake Benedict Matias na Amos Charles wa Pwani na kujinyakulia medali ya dhahabu katika mashindano ya UMISSETA yanayoendelea mjini Mtwara

Mwanariadha Thereza Bernard (kulia) akimaliza mbio za mita 200 huku akichuana kwa karibu na Emmy Hosea wa Singida na Hermegrida Manifred wa Pwani walioshika nafasi ya pili na ya tatu katika fainali za mbio hizo zilizokamilika leo asubuhi mjini Mtwara

Mwanariadha Japhet Joseph wa Singida akimaliza mbio za mita 800 na kuibuka bingwa wa mbio hizo mara baada ya kuwaacha kwa nyuma wenzake Abrahamu chapa wa Morogoro aliyeshika nafasi ya pili na William Mguya wa Manyara ambaye alishika nafasi ya tatu katika fainali hizo zilizofanyika leo asubuhi mjini Mtwara

*******************

Na Mathew Kwembe, Mtwara

Mwanafunzi Ismail Hussein Tosiri kutoka shule ya sekondari Makongo ya jijini Dar es salaam, amefanikiwa kunyakua medali ya dhahabu kwa upande wa wavulana kwenye fainali ya mashindano ya Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari (UMISSETA)  iliyofanyika leo katika viwanja vya chuo cha ualimu Mtwara.

Ismail ambaye pia ni bingwa wa riadha kwa nchi za Afrika Mashariki kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 21 aliwaacha kwa mbali wanariadha wenzake Benedict Matias  kutoka Pwani ambaye alishika nafasi ya pili na Amos Charles  pia wa pwani ambaye alishika nafasi ya tatu.

Licha ya kukiri kuwa mashindano ya mwaka huu yalikuwa magumu kwake kutokana na ushindani wa hali ya juu uliojitokeza kwenye mbio hizo, Ismaili alijigamba kuwa siri ya mafanikio yake ni mazoezi makali aliyokuwa anayafanya kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.

Amesema kuwa hivi sasa anajipanga vema ili aweze kufanya vizuri kwenye mashindano ya ya shule za Sekondari Afrika Mashariki FEASA yaliyopangwa kufanyika mkoani Arusha mapema mwezi wa nane mwaka huu.

 Kwa upande wa wasichana bingwa wa mbio za mita 200 ni Thereza Bernard kutoka Simiyu ambaye aliwashinda wenzake Emmy Hosea kutoka Singida aliyeshika nafasi ya pili na Hermegrida Manifred kutoka Pwani alishika nafasi ya tatu.

Katika fainali za mita 800, bingwa wa mbio hizo mwaka huu kwa upande wa wavulana ni mwanafunzi Japhet Joseph kutoka Singida ambaye alijinyakulia medali ya dhahabu, nafasi ya pili imeshikwa na Abrahamu Chapa wa Morogoro aliyejinyakulia medali ya fedha na medali ya shaba imekwenda kwa William Mguya kutoka Manyara ambaye alishika nafasi ya tatu.

Katika fainali za mita 800 wasichana, nafasi ya kwanza imechukuliwa na mwanariadha Gaudensia Manero kutoka mkoa wa Pwani, nafasi ya pili imechukuliwa na Rahel Nira wa Simiyu na nafasi ya tatu imekwenda kwa Regina Deogratius wa Pwani.

Kufuatia kukamilika kwa mbio hizo, mjumbe wa kamati ya ufundi wa chama cha riadha Tanzania Robert Kalyahe alisema kuwa wanariadha walioshindana katika mbio za mita 200 na 800 mwaka huu walishindwa kufikia viwango vya mwaka jana na miaka iliyopita kwa vile wengi wa waliokuwa wakishiriki mashindano hayo ni wapya kwa vile wazoefu wengi wamekwishamaliza elimu yao ya sekondari.

Kadhalika amesema kuwa wanafunzi wengi walioshiriki mbio hizo mwaka huu walikimbia bila ya kuwa na viatu jambo ambalo amesema kuwa siyo sawa kwani limewanyika ushindi vijana wengi waliokuwa na vipaji.

“Wanariadha walioshinda wengi wao walikuwa na viatu vya kukimbilia (spikes) ambavyo kariakoo bei yake haizidi shilingi 30,000, ukilinganisha na viatu vinavyotumiwa na wacheza mpira wa miguu ambavyo ni karibu shilingi 90,000, “ amesema Kalyahe, na kuongeza:

“Jamii inapaswa kuwekeza kwenye mchezo wa riadha kama kweli tunataka kurudisha heshima ya mchezo huu kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ya ushiriki wa kina Nyambui, na Bayi.”

Kalyahe amesema kama kweli tunataka kushinda kimataifa jukumu la kutafuta vipaji vya wanamichezo wanariadha linapaswa kwenda hadi vijijini badala ya kuishia kwenye akademi za michezo.