Home Mchanganyiko DKT. MABODI AMEWATAKA WANACHAMA KUHAKIKISHA WANASHINDA MAJIMBO YOTE YA UCHAGUZI WILAYANI MFENESINI

DKT. MABODI AMEWATAKA WANACHAMA KUHAKIKISHA WANASHINDA MAJIMBO YOTE YA UCHAGUZI WILAYANI MFENESINI

0

 

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi,akivishwa Skafu na Kijana wa UVCCM wa Wilaya ya Mfenesini Unguja mara baada ya kuwasili katika Ukumbi wa Mikutano wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Magharibi ”A” Unguja, kwa ajili ya kufungua Mkutano wa kawaida wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Wilaya ya Mfenesini Unguja.

NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla Mabodi,akipokea Heshima ya Utii kutoka kwa Vijana Maalum wa UVCCM Wilaya ya Mfenesini mara baada ya kukagua Gwaride la Kikundi hicho alipowasili katika ukumbi wa Mikutano kwa ajili ya kufungua Mkutano wa Kawaida wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Mfenesini Unguja

MWENYEKITI wa CCM Wilaya Mfenesini Ndugu Kesi Mashaka Ngusa akizungumza katika Mkutano wa kawaida wa Halmashauri Kuu ya Wilaya hiyo uliofanyika leo huko katika ukumbi wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja

MWENYEKITI wa CCM Mkoa Magharibi Ndugu Mohamed Rajab Soud akizungumza katika Mkutano wa kawaida wa Halmashauri Kuu ya Wilaya hiyo uliofanyika leo huko katika ukumbi wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja.

*****************************

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi,amewataka Wanachama,Viongozi na Watendaji wa CCM Wilaya ya Mfenesini kuhakikisha Taasisi hiyo inashinda Majimbo yote ya Uchaguzi ndani ya Wilaya hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa Dola Mwaka 2020.

Kauli hiyo ameitoa leo wakati akifungua Mkutano wa kawaida wa Halmashauri Kuu ya Wilaya hiyo uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Baraza la Manispaa ya Wilaya ya Magharibi ‘A’ Unguja.

Alisema Viongozi na Watendaji hao kwa kushirikiana na Wanachama na Makada  mbali mbali wanatakiwa kuendelea kufanya kazi mbali mbali zikiwemo kuelezea kwa kina namna Ilani ya CCM ya mwaka 2015/2020 inavyotekelezwa katika maeneo yao.

Aliwataka viongozi hao kuendeleza mikakati ya kuongeza Wanachama wapya waliotimiza umri wa kupiga kura kwa mujibu wa Sheria za Nchi, ambao ndio Mtaji wa kudumu wa CCM watakaoleta ushindi wa Chama katika Uchaguzi Mkuu wa Dola Mwaka 2020.

Katika maelezo yake Dk.Mabodi,alisema Serikali ya Awamu ya Saba chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, amekuwa ni kinara wa kuenzi na kudumisha Amani na Utulivu wa Nchi hali inayochochea Maendeleo Endelevu.

Alieleza kuwa Tunu hiyo ya Amani inatakiwa kulindwa kwa gharama yoyote na kila Mwananchi bila kujali tofauti za Kidini,Kisiasa na Kikabila kwani ndio chimbuko la mafanikio katika Nyanja mbali mbali za Kiuchumi,Kijamii na Kisiasa.

“CCM tunaendelea kusimamia Serikali yetu itekeleze kwa kasi Ilani ya Uchaguzi kama tulivyoahidi wakati wa Kampeni za kuomba ridhaa za Uongozi kutoka kwa Wananchi,tumepiga hatua kubwa ya maendeleo katika Sekta mbali mbali za Kilimo,Uvuvi,Afya,Mawasiliano,Usafiri wa Anga,Baharini na Nchi kavu,Elimu na Barabara”,alisema Dk.Mabodi.

Dk.Mabodi alieleza kwamba Chama Cha Mapinduzi kinawathamini Wananchi Wote bila kujali tofauti zao za Kisiasa ndio maana kinasimamia Sera zake zitekelezwe kila eneo linalohitaji huduma za Kijamii na Kiuchumi.

Sambamba na hayo aliwasihi Viongozi hao kuendeleza Utamaduni wa kufanya Vikao vya Kikatiba kwa Wakati husika ili kutoa fursa pana ya ngazi mbali mbali za Uongozi kujadili na kufanya Maamuzi ya kuimarisha Chama.

Aliwakumbusha kwamba CCM haitovumilia Mwanachama yeyote atayetumika kufanya ama kufanyiwa kampeni za kugombea nafasi za Uongozi mwaka 2020,kabla ya Chama kutangaza kufanyika kwa mchakato huo.

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi Ndugu Mohamed Rajab Soud,alisema kufanyika kwa Mkutano huo kunatoa nafasi pana kwa Ngazi ya Mkoa ya Kichama kufanya kazi zake kwa ufanisi.

Alisema kuwa Hali ya Kisiasa ndani ya Mkoa huo kwa sasa ipo vizuri na inaimarika zaidi kutoka na juhudi za Viongozi wa Majimbo ambao ni Wabunge na Wawakilishi kutekeleza Wajibu wao kwa Jamii.

Kwa upande Wake Mwenyekiti wa Wilaya ya Mfenesini Ndugu Kesi Mashaka Ngusa,alisema Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo imeendelea kutekeleza kwa ufanisi masuala mbali mbali ya kuleta Maendeleo ndani ya Wilaya sambamba na kuwajenga Kiitikadi na Kiuongozi Wanachama wa CCM hasa Vijana na Wanawake.