Ofisi ya Makamu wa Rais inapenda kuujulisha Umma wa Watanzania kuwa Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za Kupiga Marufuku Mifuko ya Plastiki za Mwaka 2019 zimeanza kutekelezwa kuanzia tarehe Mosi Juni 2019.
Baada ya kuanza kwa utekelezaji wa Katazo la Kutumia mifuko ya Plastiki baadhi ya wazalishaji na wasambazaji wamebadilisha mifuko laini ya plastiki isiyokuwa na mishikio na kuitumia kama vibebeo vya bidhaa. Hii ni kinyume na kanuni ya 8 ya Kanuni tajwa hapo juu.
Kanuni ya 9 inatoa msamaha kwa baadhi ya vifungashio vya plastiki kwa ajili ya huduma za afya au ambavyo vinatumika kwenye kufungashia bidhaa za viwandani au sekta ya ujenzi au sekta ya kilimo au vyakula au usafi na udhibiti wa taka. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) linaandaa viwango vya Vifungashio hivi ambavyo vitaainisha kiwango cha unene na uwekwaji wa lakiri na kutambulisha bidhaa iliyofungashwa kabla ya kuuzwa.
Ofisi ya Makamu wa Rais inautahadharisha Umma kuwa ni makosa kisheria kubadili matumizi ya vifungashio hivyo kuwa mifuko ya kubebea bidhaa. Adhabu stahiki zitatolewa kwa watengenezaji, waingizaji, wasambazaji na watumiaji wa vifungashio vya plastiki vilivyozalishwa ama kuingizwa nchini na kutumika kama vibebeo vya bidhaa.
Utunzaji na Usimamizi wa Mazingira ni jukumu letu sote.