Home Mchanganyiko DC ASIA ABDALAH – RAIS DKT MAGUFULI AMETEKELEZA MIRADI MINGI YA MAJI...

DC ASIA ABDALAH – RAIS DKT MAGUFULI AMETEKELEZA MIRADI MINGI YA MAJI AMBAYO HAIJAWAHI KUTEKELEZWA KILOLO

0

*********************

Mkuu wa wilaya ya Kilolo mkoani Iringa Asia Abdalah amesema kuwa toka wilaya ya Kilolo imeanzishwa na toka nchi ipate uhuru hakuna kipindi ambacho wilaya hiyo imekuwa na miradi mingi ya maji kama kipindi hiki kinachoongozwa na Rais Dkt John Magufuli, mwandishi Francis Godwin anaripoti kutoka Kilolo.

Akizungumza leo baada ya kukagua mradi wa tanki la maji kwa ajili ya kutatua kero ya maji mji wa Ilula ,mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa ujenzi wa mradi huo mkubwa wa maji utasaidia kumaliza kero ya maji ambayo wamekuwa wakiipata wananchi wa mji wa Ilula .

” Huu ni mradi mkubwa wa maji ambao utawanufaisha wananchi wa kata ya Ilula na kata nyingine za ukanda huu wa Ilula ambao walikuwa wakipata tabu ya maji ” alisema Asia

Kuwa ujenzi wa mradi huo wa maji Ilula unaendelea vizuri na kuwa wakati wa ziara ya mkuu wa mkoa wa Iringa Alli Hapi kwa ajili ya kukagua mradi huo alikuwa ametoa maelekezo ambayo yamefanyiwa kazi na sasa mradi unaendelea vizuri .

Alisema kuwa mbali ya mradi huo utakaowanufaisha wakazi wa Ilula wilaya ya Kilolo ina miradi mingine saba na kufanya jumla kuwa na miradi mikubwa nane ya maji ambayo itakuwa ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa wilaya ya Kilolo.

Pia alisema pamoja na miradi hiyo kuna miradi mingine mitatu mikubwa ya maji iko mbioni kujenga hivyo iwapo miradi hiyo itakamilika uwezekano wa wananchi wa wilaya hiyo kukabiliwa na changamoto ya maji itabaki kuwa historia .

Mkuu huyo alisema kuwa mradi huo ambao unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 5 ambazo ni kodi za watanzania umefikia asilimia 45 kukamilika na kuwa ujenzi wa tanki pekee umefikia zaidi ya asilimia 90 .

Alisema kuwa mradi huo umeendeshwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ulitengewa bilioni 5 na awamu ya pili utatumia kiasi cha Tsh bilioni 4 hadi kukamilika kwake .

Akizungumzia kuhusu utunzaji wa mradi huo na miradi mingine ya maji wilayani Kilolo mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kuendelea kutunza mazingira ili kuifanya miradi hiyo kuwa endelevu na kuwa elimu ya utunzaji mazingira imeendelea kutolewa na wilaya hiyo imezidi kupata tuzo mbali mbali za utunzaji mazingira.