Home Mchanganyiko BI.BELINDA ANUSURIKA KIFO BAADA YA KUJIFUNGUA NA KUTOKWA DAMU NYINGI WILAYANI RORYA,MKOANI...

BI.BELINDA ANUSURIKA KIFO BAADA YA KUJIFUNGUA NA KUTOKWA DAMU NYINGI WILAYANI RORYA,MKOANI MARA

0

Aliyebeba Mtoto ni Binti aliyenusurika kifo Bi.Belinda Nashoni Pembeni yake ni mumewe  kushoto kwake nguo nyeupe ni muuguzi aliyenusuru maisha ya Binti huyo Nangi Mgoni Muuguzi mkunga Zahanati ya nyancha bakenye  kulia kwake ni mganga mfaiwidhi kituo cha nyanchabakenye  Dkt. Burasius Mganyizi,na Mratibu wa huduma ya mama na mtoto Rorya Neema mwijarubi kushoto kwake mama mkwe. wa Belinda.

………………….

Na Mussa John   MARA

Mkazi wa kijiji cha Marasibora katika wilaya ya Rorya mkoani Mara Belinda Nashon (19) amenusurika kifo kutokana na juhudi binafsi zilizofanywa na wahudumu wa afya  baada ya kujifungua na kutokwa damu nyingi .

Tukio hilo lilitoke Mei  24 mwaka huu katika zahanati ya kijiji cha Nyanchabakenye kata ya Kisumwa wilayani Rorya ambapo mama huyo alifika kwaajili ya kujifungua majira ya saa 12 jioni.

Akieleza jinsi tukio hilo lilivyotokea Afisa  Muuguzi mkunga wa zahanati hiyo,  Nangi Mgomi alisema kuwa baada ya mama huyo kufika katika zahanati hiyo na kufanyiwa uchunguzi ilugundulika kuwa na uchungu hivyo alikadiriwa kujifungua majira ya saa 3 usiku.

” Ilipofika saa 3 kweli alijifungua mtoto wa kiume chini ya uangalizi wangu lakini ghafla alianza kutoka damu nyingi hadi kupoteza fahamu na kwa muda huo nilikuwa mwenyewe kwasababu hii ni zahanati ambapo huwa kuna muda wa kufunga isipokuwa huduma za dharura kama kujifungua huwa tunatoa ” alisema Muuguzi huyo.

Alisema kuwa baada ya kuanza kutoka damu alijitahidi kutoa huduma kitaalam kwaajili ya kuzuia damu hizo na kwamba kadri muda ulivyokuwa ukienda ndivyo hali ilivyokuwa inazidi kuwa mbaya na hivyo kulazimika kuwasiliana na kitengo cha gari la wagonjwa kutoka katika kituo cha afya cha Utegi kilichopo zaidi ya kilomita 40 kutoka zahanati hiyo.

” Nilimuomba mke wangu atafute kwenye simu yangu namba ya muhusika na aipige halafu aniwekee simu masikioni ili niongee naye kwavile mikono yangu ilikuwa imejaa damu huku nikijitahidi kufanya kila niwezalo ili kunusuru maisha ya mama huyo ambayo kwa muda huo yalikuwa katika hatari kubwa” alisema Mgomi

Aliendela kufafanua  kuwa baada ya kumpata mtu wa gari la wagonjwa aliambiwa kuwa gari hilo halikuwa na mafuta hivyo lisingeweza kufika katika eneo hilo jibu ambalo lilififisha matumaini yake ya kuokoa maisha ya mama huyo kabla ya kumpigia simu mratibu  wa afya ya uzazi na watoto wa wilaya hiyo ambaye alimpa matumaini tena.

” niliona kama mama ananifia mikononi huku naona na sina cha kufanya ndipo nikakumbuka kuwasiliana na mratibu ingawa ilikuwa ni usiku lakini aliniahidi kuwa angefanya kila awezalo ili waweze kufika na tuweze kumkimbiza mama huyu katika hospitali ya Kowak kwa matibabu zaidi na kweli aliweza kufanya hivyo na kufika hapa majira ya saa 5 usiku” alisema Muuguzi huyo

Alisema kuwa hili ni tukio la tatu la aina hiyo kutokea katika zahanati hiyo katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu huku akisema kuwa matatizo kama hayo huwa hutokea kwasbabaua mbalimbali ikiwemo matumizi ya dawa za kienyeji kwa wamama wajawazito sambamba na sababu zingine za kitaalam.

Naye mratibu wa afya ya uzazi na mtoto wilaya ya Rorya, Neema Mwijarubi alisema kuwa baada ya kupokea simu ya dharura kutoka kwa Muuguzi huyo alifanya jitihada za kutafuta mafuta ili kuweka kwenye gari hilo na kufika katika zahanati hiyo huku akieleza kuwa matumaini ya kuokoa maisha ya mama huyo yalikuwa ni madogo kutokana na kutokwa na damu nyingi nankisha kupoteza fahamu.

” Nilitafuta hela binafsi na kuweka mafuta ila tulipofika zahanati kwakweli hali ilikuwa mbaya sana maana mama alikuwa amebadilika na kuwa mweupe kutokana na kutokuwa na damu baada ya kutokwa na damu nyingi sana” alisema Neema

Alisema kuwa ingawa kulikuwa na mvua kubwa lakini walijitahidi kumuwahisha katika hospitali ya Kowak ambapo mara baada ya kuwasili tu walipokelewa na kupewa huduma za dharura kutokana na maandalizi yaliyokwisha kufanyika baada ya kupiga simu hospitalini hapo  na kutoa taarifa juu ya mama huyo wakiwa njiani

Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake mama huyo (Belinda) alisema kuwa anaamini bila jitihada hizo hivi sasa asingekuwepo duniani.

Alisema kuwa kabla ya kupoteza fahamu alishuhudia namna ambavyo Muuguzi huyo alivyokuwa akijitahidi kadri ya uwezo wake kuhakikisha kuwa anayaokoa maisha yake baada ya kujifungua na kuanza kutokwa damu lakini baadaye hakuweza kujua nini kilichoedelea hadi pale alipopata fahamu akiwa katika hospitali ya Kowak  majira ya saa 9 usiku.

Kufuatia hali hiyo Mkuu wa mkoa wa Mara, Adam Malima aliwapongeza wahudumu haonkwa jitihada binafsi wakizozifanya hadi kuokoa maisha ya mama huyo pamoja na mtoto wake.

Alisema kuwa uongozi wa mkoa Mara umefurahishwa na kitendo hivho na kuamua kuwapa motisha ya sh 1 milioni pamoja na vyetu kama njia ya kitambua mchango wao huku akisisitiza uwajibikaji kwa watumishi wa idara ya afya mkoani Mara katika kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa tatizo la vifo vitokanavyo na uzazi.

” kitendo hiki ni cha kupongezwa sana na kinafaa kuigwa na kila mmoja wetu, tunapaswa kuthamini uhai wa akina mama maana hakuna anayepaswa kupoteza maisha akiwa analeta kiumbe duniani na kwetu sisi kila uhai una thamani kubwa sana nawashukuru sana hawa walioonyesha kwa mfano walipambana hadi usiku wa manane pamoja na mazingira magumu kuhakikisha kuwa huyu mama mmoja anapona ” alisema Malima.

Naye mganga mfawidhi wa zahanati hiyo Dk.  Brasius Muganyizi alisema kuwa pamoja na huduma wanazozitoa zipo changamoto nyingi zinazowakabili hivyo kufanya utoaji wa huduma kuwa mgumu.

Alisema kuwa zaidi ya akinamama 30 hujifungua katika zahanati hiyo kwa mwezi  huku kukiwa na upungufu mkubwa wa vifaa tiba ikiwemo vitanda na wodi za kuwalaza akinamama mara baada ya kujifungua.

Alisema kuwa hivi sasa wanalazimika kuwalaza kwenye chumba cha kutolea chanjo huku wakiwa na vitanda viwili tu jambo ambalo limekuwa likiwalazimu kwenda kinyume cha utaratibu wa kumuhudumia mama na mtoto baada ha kujifungua

” kawaida mama anatakiwa kuwa chini ya uangalizi kwa muda wa saa 24 baada ya kujifungua lakini kutokana na kukosekana kwa wodi na vitanda sisi hapa tunawaruhusu hata baada ya saa mbili baada ya kujifungua inapotokea kuna mama mwingine anahitaji kujifungua hivyo tunaomba mamlaka husika zitusaidie kuboresha miundombinu sambamba na kupatikana kwa vifaa tiba ” Alisema mganga huyo