Home Mchanganyiko TEMESA SINGIDA YAAGIZWA KUTUMIA VIZURI RASILIMALI WATU

TEMESA SINGIDA YAAGIZWA KUTUMIA VIZURI RASILIMALI WATU

0

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle kulia akikagua jengo jipya la karakana ya Wakala huo mkoani Singida aliloagiza lijengwe wakati wa ziara yake aliyoifanya kwenye karakana hiyo mwishoni mwa mwaka jana.  Kushoto ni Kaimu Meneja wa TEMESA Singida Mhandisi Saidi Muhindi.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle akitoka kukagua jengo jipya la ofisi kwa ajili ya wafanyakazi wa karakana ya TEMESA mkoa wa Singida ambalo aliagiza lijengwe mwishoni mwa mwaka jana na ujenzi wake umekamilika hivi karibuni.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle (wa pili kulia) akitoa maagizo wakati akikagua karakana ya Wakala huo mkoani Singida. Kulia ni Kaimu meneja mkoa wa Singida Mhandisi Saidi Muhindi.

PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (TEMESA SINGIDA)

 ………………

ALFRED MGWENO (TEMESA) SINGIDA

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Y. Maselle mwishoni mwa wiki hii ametembelea karakana ya Wakala huo mkoa wa Singida na kumuagiza kaimu meneja kujitahidi kutumia vizuri rasilimali watu alizonazo katika mkoa wake ili kuongeza ufanisi wa karakana.

Mapema katika ziara hiyo Mhandisi Maselle aliitisha kikao kifupi na watumishi ambapo Kaimu meneja Mhandisi Saidi Muhindi alizungumza kwa niaba yao na kuzungumzia changamoto mbalimbali walizonazo katika karakana hiyo mojawapo ikiwemo ya upungufu wa watumishi wa karakana na kumuomba Mtendaji mkuu kufikiria kuwaongezea watumishi ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi. Mhandisi Muhindi alisema, ‘’upande wa karakana tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi, wako mafundi watatu tu na mmoja yuko likizo, kazi zinazoingia ni nyingi hivyo tunazidiwa sana’’.

Akiitolea ufafanuzi changamoto hiyo, Mhandisi Maselle alisema haitawezekana kupata watumishi wengi kwa mkupuo na kuwasambaza katika karakana zenye upungufu wa wafanyakazi kwa mara moja hivyo akamtaka meneja huyo kuwatumia wale wachache alionao vizuri wakati akiangalia namna ya kuajiri wafanyakazi wengine.

‘’Haitakuwa rahisi kukuletea watumishi ishirini au hamsini kwa pamoja, kwa sasa Wakala unaangalia uwezekano wa kukupa watumishi wachache katika wale walioajiriwa hivi karibuni kupitia sekretarieti ya ajira, lakini tumia vizuri hawa ulionao hasa wazee wazoefu, wakae na vijana wawafundishe na naamini kazi zitafanyika vizuri”. Alijibu Mhandisi Maselle.

Aidha, Kaimu meneja Mhandisi Saidi Muhindi alimpitisha Mtendaji mkuu kujionea jengo jipya la ofisi ya karakana ambalo aliagiza lijengwe wakati alipofanya ziara mkoani humo mwishoni mwa mwaka jana ambalo tayari limekamilika na wakati wowote kuanzia sasa litaanza kutumiwa na watumishi hao.

Vilevile katika ziara hiyo, Mhandisi Maselle pia alimuagiza meneja huyo kuhakikisha anakuwa na akiba ya kutosha ya vipuri hasa vipuri vya matengenezo ya kinga (fast moving items) ambavyo huwa vinatoka mara kwa mara) katika karakana hiyo ili kuepuka kufuata vipuri katika maduka ya watu binafsi na hivyo kuchelewesha matengenezo ya magari.