Home Mchanganyiko NEC YAKABIDHI ORODHA YA VITUO KWA VYAMA VYA SIASA

NEC YAKABIDHI ORODHA YA VITUO KWA VYAMA VYA SIASA

0

NA SULEIMAN MSUYA

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imegawa daftari la orodha ya vituo vya kuandikisha wapiga kura kwa vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu.

Zoezi hilo la ugawaji wa daftari hilo la orodha ya vituo limefanyika jijini Dar es Salaam ambapo vyama vyote vya siasa vilishiriki.

Akizungumzia mchakato huo Mwenyekiti wa NEC Jaji Semistocles Kaijage alisema katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2020 tume chini ya Ibara ya 74(6) ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 imepewa mamlaka ya kutekeleza majukumu yake mbalimbali ya msingi ikiwa ni pamoja na kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Rais na  wabunge Jamhuri ya Muungano Tanzania na madiwani Tanzania Bara.

“Kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Kifungu cha 21(5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Sura ya 292 tume inapaswa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura mara mbili katika uchaguzi mkuu mmoja na uchaguzi mwingine unaofuta.

Napenda kuwataarifu kuwa tume imekamilisha sehemu kubwa ya maabdalizi ya uboreshaji ambapo uhakiki wa vituo vya kujiandikisha, uandikishaji wa majaribio, upangaji wa ratiba na mkakati wa elimu ya mpiga kura,” alisema.

Jaji Kaijage alisema tume inatarajia uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura mwezi Julai 2019 kwa kutumia teknolojia ya kieletroniki ya biometriki ambayo inachukua taarifa za mtu kibaiolojia na kuzihifadhi katika kanzidata kwa ajili ya utambuzi.

Alisema uboreshaji wa sasa hautahusisha wapiga kura wote waliondikishwa mwaka 2015 na kwamba utawahusu wapiga kura wapya waliotimiza miaka 18 na zaidi au wataotimiza  umri huo siku ya uchaguzi.

“Kundi lingine litakalohusika ni watakaoboresha taarifa kama vile waliopoteza  kadi au kadi kuharibika, wanaoboresha taarifa na waliohama.

Alisema daftari hilo walilokabidhiwa vyama vya siasa limeanisha vituo vyote ambavyo vitahusika na uandikishaji wa wapiga kura wenye sifa.

Jaji Kaijage alisema tume imeongeza vituo vya kujiandikisha kutoka 36,549 hadi 37,407 kwa upande wa Tanzania Bara.

“Zanzibar vituo vilikuwa 380 kwa sasa vitakuwa 407 hivyo vitarahisisha mchakato wa uboreshaji daftari,” alisema.

Mwenyekiti huyo alisema pia  tume kupitia kifungu cha 4C inaendelea kutoa elimu ya mpiga kura kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Alisema katika kufanikisha hilo NEC imeanza kukutana na wanasiasa, asasi za kirai, viongozi wa dini, makundi maalum na wadau wengine kuanzia ngazi ya taifa na mkoa.

Aidha, Jaji Kaijage kuhusu utekelezaji wa hukumu ya makamaka kuu kuzuia wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi alisema tume itatekeleza maamuzi yoyote ambayo yapo kisheria kama yanavyotaka.

Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dk.Athumani Kihamia, alisema tume imejipanga kushirikiana na wadau ili kuondoa malalamiko huku akisisitiza sio lazima kufuata kila jambo wanaloambiwa au kushauriwa.

Alivitaja vyama vya siasa kuzingatia Sheria, kanuni na taratibu zilizopo kwenye Sheria ya uchaguzi ili waweze kuenda sawa.

Akizungumzia mkutano huo Katibu wa Kampeni na Uchaguzi Chama cha ACT Wazalendo Masaga Masaga alisema utoaji wa daftari ni jambo zuri ili vyama viweze kujua.

Masaga alisema pamoja na kukabidhiwa daftari wanaiomba tume itekeleze hukumu ya mahakama kuu kuhusu wasimamizi kutosimamia uchaguzi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Chama cha Wananchi CUF, Jafar Mneke alisema NEC imekiuka Sheria kwa kushindwa kuboresha daftari mara mbili  kabla ya uchaguzi.

Katika mkutano huo vyama vyote 19 vilituma wawakilishi ambavyo ni Chadema, CUF, CCM, ACT Wazalendo, Chauma, AFF, NLD, DP, UPDP, TLP, NCCR Mageuzi, NRA, CCK, SAU, UMD, ADC, UDP na Demokrasia Makini.