Na Mwandishi Wetu.
BEKI wa Simba SC, Shomari Kapombe na viungo Jonas Mkude, wote wa Simba na Ibrahimu Ajibu wa Yanga wameenguliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars kinachoondoka leo kwenda Misri kwa kambi ya mwisho ya kujiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zikazofanyika baadaye mwezi huu nchini Misri.
Wengine walioenguliwa ni Kennedy Wilson wa Singida United, Ally Ally wa KMC, Khamis Khamis wa Kagera Sugar na Ayoub Lyanga wa Coastal Unon ya Tanga.
Taifa Stars inaondoka na wachezaji 32 kwenda kambini mjini Alexandria, Misri baada ya kuchujwa saba na kati ya hao ni 23 tu watashiriki AFCON.
Wachezaji wengine wataendelea kubaki kambini kwa maandalizi ya michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.
Kikosi cha kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike kitaanza na mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji wa AFCON, Misri Juni 13, mwaka huu Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria.
Baada ya hapo Taifa Stars itacheza mechi zake tatu za Kundi C mfululizo ikianza na Senegal Juni 23, Kenya Juni 27 na kumaliza na Algeria Julai 1 kuangalia matokeo yake kama yataipeleka hatua ya mtoano.
Kikosi cha Taifa Stars kinachoondoka kinaundwa na makipa; Aishi Manula (Simba SC), Metacha Mnata (Mbao FC), Suleiman Salula (Malindi SC) na Aaron Lulambo (Tanzania Prisons).
Mabeki; Claryo Boniface (U20), Hassan Kessy (Nkana FC, Zambia), Vincent Philipo (Mbao FC), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni (Simba SC), Kelvin Yondan, Gardiel Michael (Yanga SC), Abdi Banda (Baroka FC, Afrika Kusini), Ally Mtoni (Lipuli FC), David Mwantika na Aggrey Morris (Azam FC).
Viungo ni Feisal Salum, Himid Mao (Petrojet, Misri), Frank Domayo, Mudathir Yahya (Azam FC), Shiza Kichuya (ENNPI, Misri), Simon Msuva (Difaa Hassan El-Jadidi Morocco), Farid Mussa (Tenerife, Hispania) na Freddy Tangalu (Lipuli FC).
Washambuliaji ni Yahya Zayd (Ismailia, Misri), Shaaban Iddi Chilunda (Tenerife, Hispania), Rashid Mandawa (BDF, Botswana), Miraj Athumani (Lipuli FC), Kelvin John (Serengeti Boys), Adi Yussuf (Solihull Moors, England), John Bocco (Simba SC), Thomas Ulimwengu (JS Saoura, ALgeria) na Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji).