Waziri wa Habari Utamaduni,Sanaaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Klabu ya Dar es Salaam Young Africans (Yanga) uliofika kijitambulisha ofisini kwake Jijini Dododma leo Juni 04,2019.
*****************************************
Shamimu Nyaki-WHUSM
Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe ameutaka uongozi mpya wa Klabu ya Dar es Salaam Young Africans (Yanga) kufanya kazi kwa weledi na ubunifu katika kuiletea mafanikio klabu hiyo pamoja na kuhakikisha maslahi ya timu hiyo yanalindwa.
Mhe. Mwakyembe ameyasema hayo leo Jijini Dodoma alipokutana na Uongozi wa Klabu hiyo ulioongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Mshindo Msolla ambao ulikuja kujitambulisha rasmi kwa Waziri.
“Nawapongeza sana kwa kuaminiwa na wanachama pamoja na wapenzi wa Klabu hii ambayo ina historia kubwa katika soka hapa nchini hivyo ni jukumu lenu kuhakikisha timu hii inaendelea kufanya vizuri ndani na nje ya nchi” Mhe. Mwakyembe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu hiyo Prof. Mshindo Msolla ameishukuru Serikali kwa msimamo wake wa kuhakikisha klabu hiyo inaendelea kusimama licha ya kukaa muda mrefu bila uongozi rasmi pamoja na kusaidia kutatua mgogoro uliokuwepo ndani ya klabu hiyo.
Prof. Msolla ameongeza kuwa Klabu hiyo inatarajia kufanya hafla ya kuichangia klabu itakayofanyika tarehe 15,juni 2019 Jijini Dar es Salaam ambapo amewataka wanachi na wapenzi wa klabu kujitokeza katika hafla hiyo.